Update:

18 August 2016

Masanja atafutwa kina Joti wakidhaminiwa

Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salam linamtafuta Emmanuel Mgaya 'Masanja Mkandamizaji'baada ya kuwakamata ,kuwahoji na kuwaachia kwa dhamana waigizaji wenzake wanne wa kundi la Original Comedy kwa kosa la kuvaa sare za jeshi hilo jijini

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kundi hilo lilivaa nguo zinafonana na sare ya polisi wakati wa harusi ya Masanja Mkandamizaji.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Hezron Gyimbi, aliwaambia waandishi wa habari jijini jana kuwa wasanii hao walikamatwa juzi saa 10 jioni.
Aliwataja waigizaji waliokuwa wakishikiliwa na jeshi kabla ya kupatiwa dhamana jana kuwa ni Lucas Lazaro (Joti), Serious David, Alex John na Isaya Gideon.
Gyimbi alisema wanamtafuta Masanja kwa ajili ya mahojiano baada ya kutokuwa mmoja wa wasanii waliokamatwa juzi.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa kosa la kuvaa sare zinazodhaniwa kuwa ni za Jeshi la Polisi. Alizitaja sare hizo kuwa ni kofia, suruali, shati, mikanda, filimbi na beji yenye cheo cha polisi.
Alisema kukamatwa kwa wasanii hao kumelenga kujua walikozipata sare hizo, uhalali wa kuwa nazo pamoja na kuchunguza kama wana vifaa vingine vya jeshi hilo mbali ya hivyo walivyoonekana navyo.
Gyimbi alisema wasanii hao watakuwa nje wakati upelelezi ukiendelea na watakuwa wanahitajika Polisi kwa ajili ya mahojiano wakati wowote.
Video za waigizaji hao wakiwa na nguo zinazodaiwa na Jeshi la Polisi kuwiana na sare zao, zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha wakitoa burudani kwenye harusi ya Masanja.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo pia lilimuhoji Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, na mwandishi wa gazeti la Mwanahalisi, Josephat Isango, jana kuhusu habari mbalimbali walizozichapisha katika gazeti la Mwanahalisi hivi karibuni.
Agosti 15, mwaka huu, Kubenea aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa juu ya makala iliyochapishwa kwenye gazeti hilo wiki tatu zilizopita, ikielezea hali ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu Zanzibar.
Gyimbi alisema wawili hao waliitwa kuhojiwa kutokana na machapisho mbalimbali waliyoyatoa katika gazeti hilo linalomilikiwa na Kubenea.
Alisema Kubenea na mwandishi wake wapo nje kwa dhamana huku upelelezi ukiendelea na kwamba wataendelea na uchunguzi na muda wowote watahitajika kituoni hapo.
Isango alihojiwa pia kituoni hapo juzi kwa zaidi ya saa sita na baadaye kuachiwa kwa dhamana kuhusu habari aliyoiandika kwenye gazeti la Mseto la Agosti 4 hadi 10, mwaka huu yenye kichwa cha habari ‘Waziri amchafua JPM