Update:

04 August 2016

Dakika za mwisho uhai wa aliyeuwawa Udom

Dakika za mwisho za Mwanafunzi wa UDOM mwaka wa kwanza wa kitovu cha sayansi Fredrick Joseph (25) aliyeuwawa na watu wasiojulikana   zimewekwa hazarani na watu waliomshuhudia

Mwanafunzi huyo aliuawa kwa kipigo mwishoni mwa wiki iliyopita na watu wanaosadikiwa kuwa wanafunzi wenzake. Wakizungumza kwa nyakati tofauti  mmoja wa wanafunzi wenzake ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema wao wamefunga chuo kwa sasa na kifo chake kilitokea wakati akitokea baa ya Carnival Pub iliyoko kwenye Kitivo cha Sayansi ya Jamii na siku hiyo kulikuwa na muziki. Alisema kabla ya kifo chake, Joseph palizuka ugomvi katika ‘pub’ hiyo lakini ulitulizwa na walinzi wa klabu hiyo. Mwanafunzi huyo alisema chanzo cha ugomvi huo ni watu aliokuwa amekaa nao kudai kuwa amewaibiwa bila kutaja waliibiwa kitu gani. “Baada ya hapo sikuona kilichoendelea nikaja kusikia tu usiku ule watu wanasema Fredrick kapigwa wakati akitokea muziki,” alisema. Naye Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika kitivo hicho, alisema alisikia kelele za mwizi lakini baada ya muda akapata taarifa kuwa aliyepigiwa kelele hizo ni Fredrick. “Nyuma ya bweni letu, Block Three, alikuwa akipenda kukaa na anavuta. Lakini kitu ambacho kilikuwa kikitushangaza yeye alikuwa anapenda kutembea na kisu na hata siku ya tukio, wenzetu walioshuhudia walisema alikuwa ana kisu lakini alitupa pembeni na kujigamba anaweza kupigana nao,” alisema. Akisimulia tukio hilo, kiongozi wa walinzi wa 'pub' hiyo, Majaliwa Mkundi, alisema ilikuwa majira ya saa nane usiku wakiwa katika doria jengo la kompyuta, walisikia kelele za "mwizi mwizi". Alibainisha kuwa walitoka na kuona watu wawili wakikimbia kuelekea waliko walinzi hao na baadaye kubadili mwelekeo na wakikimbia kuelekea bwenini. “Huwezi kujua kwa sababu ya usiku ule hatukujua kama kweli ni mwizi au wana mambo yao, tukaanza kufuatilia kwa nyuma kabla ya kufika eneo wanalopata chakula tukakuta Joseph amelala chini na kundi la wenzake linatawanyika," alisema Mkundi. “Tulichokifanya ni kumshika mkono na kumuuliza vipi lakini hakuongea. Nilipomuuliza wewe ni mwanafunzi alisema ndiyo na anatokea Block Three na nilipomtaka ataje wenzake anaoishi nao hakuweza kuwataja.” Alisema kutokana na kushindwa kuzungumza na hali yake kuwa mbaya, walipiga simu polisi ili liletwe gari kumbeba lakini gari lilikuwa Ihumwa, hivyo wakachukua bajaji hadi kituo kikuu cha polisi na polisi walimwuliza akataja majina na baada ya hapo hakuzungumza tena. “Tukaenda kuchukua gari la wagonjwa na mimi nikaonekana ndo kama ndugu nikapanda kwenye hilo gari hadi hospitali. Tulipokewa lakini wakati tunaingia kwa daktari kuhudumiwa akawa amefariki dunia,” alisema Mkundi Msimamizi wa ulinzi wa klabu hiyo, Emmanuel Meshack, alisema siku ya tukio alikuwa upande wa jikoni akiwa amesimama na wenzake na baada ya muziki kuanza, aliingia Frederick na mwenzake wakaanza kunywa pombe na kucheza huku kukiwa hakuna ugomvi wowote. “Ilipofika muda wa kufunga ndipo tukaona alaleta malumbano na mwenzake aliyekuwa naye, mimi na baunsa tukaingilia kati tukawatuliza kumbe baada ya kuondoka hapa wakaendelea na ugomvi njiani wakati wanarudi bwenini,” alisema. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mmabosasa. alisema upelelezi bado unaendelea na hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.