Update:

01 August 2016

Afande aliyevalia bikini amkamata mwizi


  
Afande aliyevalia bikini amnasa mwizi wa simu
Afisa wa polisi wa kike aliyevalia bikini amewaogofya wezi mjini Stockholm Sweden baada ya kumnasa mwizi wa simu ya mkononi kwa miereka ufukweni.
Bi Mikaela Kellner na wenzake ambao pia ni maafisa wa polisi walikuwa wametoka kazini na kufululiza hadi ufukweni kujitanua chini ya jua.
Mara wakagundua bwana mmoja aliyekuwa akinadi vitabu vya watoto yatima dakika 15 zilizotangulia alikuwa amewaibia simu ya mkononi .
Wakashtuka na kuanza kumfuata mbio ufukweni.
watu waliokuwa wakijivinjari ufukweni walidhania kuwa mwanamke huyo aliyekuwa nusura uchi alikuwa akifanya mazoezi kwa jazba ya mwaka.
''Mbona hakuenda rio kwenye mashindano ya riadha ya olimpiki?
alisikika mama mmoja akimbeza.
Kufumba na kufumbua wakashtuka binti huyo aliyekuwa amevalia Bikini ''yaani sindiria na chupi'' pekee alikuwa akikabiliana na mwanaume fulani.
Hapo ndipo walipong'amua haikuwa mazoezi, na walipopeleleza wakagundua kuwa alikuwa ni afisa polisi aliyekuwa akimbana mwizi.
Lakini kwasababu huyo mwizi alijifanya ''dume'' ilimbidi kumbwaga sakafuni kwa mieleka na mateke mazitomazito.
Waandishi wa habari waliofika katika bustani hiyo ya Ralambshov baada ya kushuhudia purukushani hiyo walipigwa na butwaa alipowaeleza kuwa alikuwa ni ''afande'' aliyekuwa kazini kumnasa mwizi.
Bi Kellner amekuwa maarufu sana baada ya picha yake akiwa na pikini kuchapishwa katika majarida ya habari nchini humo.
Chini ya saa 24 baada ya tukio huyo totoshoo huyo amepokea uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wenyeji.
Ukurasa wake wa Instagram umepata ongezeko la zaidi ya wafuasi 9,000 tayari.