Update:

27 July 2016

Wadaiwa mikopo vyuo vikuu, kuzuiwa kukopa, kwenda nje

Bodi ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu (HESLB),imetoa orodha ya kwanza ya wadaiwa 1,091 na kuwataka kujisalimisha vinginevyo watawekewa vikwazo,vikiwamo kutosafiri nje ya nchi na kutokukopeshwa na taasisi yoyote ya fedha


Kupitia tangazo la bodi hiyo lililochapishwa kwenye vyombo vya habari jana, wadaiwa hao wanakabiliwa na adhabu hizo ambazo ziko kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha bodi hiyo mwaka 2004.
HESLB ilisema wakopaji ambao hawarejeshi mikopo, wanakabiliwa na hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria na kwamba majina yao yatapelekwa katika taasisi ya kuorodhesha wadaiwa sugu na watakuwa wamejinyima fursa ya kukopeshwa na taasisi zote za kifedha nchini, zikiwamo benki na vyama vya kuweka na kukopa (Saccos).
Aidha, taarifa ya HESLB ilisema hatua nyingine ambayo inakusudia kuchukua dhidi ya wadiawa, kwa mujibu wa sheria, ni kupeleka taarifa zao za kina Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara ya Uhamiaji na balozi zote ili wanyimwe ruhusa ya kusafiri nje ya nchi.
Wadaiwa hao pia watanyimwa kupata udhamini wa serikali au kudahiliwa kwa ajili ya kusomea shahada za uzamili na uzamivu kwenye chuo chochote ndani na nje ya nchi.
Mbali na vibano hivyo vinne vitakavyoathiri mipango na mienendo ya kila siku, wadaiwa pia wanakabiliwa na hatari ya kukamuliwa fedha zaidi ya kiwango cha deni la sasa.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, wadaiwa wa HESLB watakuwa wakilipa riba ya kila mwezi ya asilimia tano ya deni la mkopo kwa kila mwaka, mbali na riba ya asilimia tano inayotozwa sasa.
Aidha, wadaiwa wa HESLB watabebeshwa gharama za kuwatafuta baada ya kukamatwa na wakala wa bodi watakaopewa kazi ya kuwafuatilia.
Kiasi cha deni la mkopo, kwa kila mmoja wa wadaiwa hao 1,091, kimeelezwa katika tangazo hilo kwenye gazeti la The Guardian kuwa kinaweza kupatikana katika ofisi za Bodi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, aliliambia gazeti hili kuwa hadi sasa mikupuo iliyoiva ambayo wanufaika wanatakiwa kulipa ni Sh. bilioni 480.
Alisema kiasi wanachodai HESLB kutoka kwa wadaiwa hulipwa kwa awamu na si kwa mkupuo na kwamba wanafanya uchambuzi wa wadaiwa na wanaolipa kila mwezi.
Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, alisema serikali itaifanyia marekebisho Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuongeza kasi ya urejeshwaji wa mikopo.
Prof. Ndalichako alisema watalazimika kuifanyia marekebisho sheria hiyo kwa kuwa kiwango cha urejeshwaji wa mikopo bado hakiridhishi.
Alisema hali hiyo inasababishwa na kuwapo kwa changamoto za kutokuwapo kwa mikakati thabiti ya ufuatiliaji wa wakopaji, udhaifu katika sheria ya muundo wa bodi hiyo.
Alisema hakuna sheria inayolazimisha marejesho ya mikopo kutokana na makato ya mishahara na mwitikio mdogo wa wanufaika kujitokeza kurejesha mikopo yao pamoja na waajiri kutotimiza majukumu yao.
"Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha wanufaika kufanya marejesho ili Watanzania wengine wenye mahitaji waweze kunufaika. Pia nawasihi wenye uwezo mdogo walipe kwa mkupuo mmoja ili kupunguza utegemezi wa Bodi ya Mikopo kwa serikali," alisema.
Aliongeza kuwa wizara yake imeongeza siku 30 katika siku 60 ilizokuwa imewapa wanufaika wa mikopo kujisalimisha lakini akaonya kinyume cha hapo majina yao yatatangazwa kwenye magazeti.