Update:

21 July 2016

Utumikishaji watoto wazidi kushamiri

Mtoto mmoja kati ya watatu Tanzania anatumikishwa katika shughuli hatarishi za kiuchumi na kwamba wanategemewa na familia kwa mahitaji ya msingi

Kadhalika asilimia 28.8 ya watoto wanatumikishwa kitaifa katika kazi za uyaya, kilimo, uvuvi na misitu, huku maeneo ya vijijini utumikishwaji ukiwa asilimia 35.6 , mijini asilimia 18 na Dar es Salaam ni asilimia 3.6.
Matokeo ya utafiti wa mwaka 2014/15, uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), ulibaini kuna watoto milioni 15 wenye umri wa miaka 5 hadi 17, wavulani wakiwa milioni 7.6 na wasichana milioni 7.1.
Maeneo ya utafiti yalikuwa 480 ambayo yaligawanywa kijiografia ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Akitoa matokeo ya utafiti huo jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Utafiti kutoka NBS, Ruth Minja, alisema watoto milioni 10.2 wako shuleni, milioni 4.4 hawako shule na milioni 2.5 hawakuwahi kwenda shule.
Alifafanua kuwa watoto milioni 4.2 ya wale ambao hawapo shuleni wako kwenye shughuli hatarishi na utumikishwaji wa zaidi ya saa 29 kwa wiki, ambayo ni kinyume cha sheria ya mtoto na mikataba ya kimataifa.
Alisema watoto walioko kwenye shughuli za kiuchumi ni asilimia 34.5, kati yao asilimia 94.3 ni wavulana na wasichana ni asilimia 89.6, huku kazi za nyumbani wasichana wakiwa asilimia 84.2 ambao wako kwenye uyaya na wanaume katika sekta hiyo ni asilimia 5.8.
“Katika shughuli za kiuchumi kigezo kilichotumika ni mazingira magumu ya kazi, kazi nzito huku kwa kazi za nyumbani ni muda wa kufanya kazi husika ambao hutumikishwa mara tatu ya muda unaotakiwa kisheria,”alifafanua.
Minja alisema watoto asilimia 4.3 wanatumikishwa zaidi ya saa zinatotakiwa na kwa ujumla robo ya watoto tatu ambayo ni asilimia 74.7 wanatumikishwa.
Aidha, alisema sababu kubwa za utumikishwaji huo ni kuhudumia familia na wengi wanatoka kwenye familia duni pamoja na malezi duni.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, alisema matokeo pia yanaonyesha kuwa watoto hutumia zaidi ya nusu ya muda wao yaani asilimia 58.8 kujihudumia na usafi binafsi, huku wasichana wakitumia asilimia 59.2 ikilinganishwa na wavulana asilimia 58.3.
“Shughuli za kujisomea kwa watoto zinachukua nafasi ya pili kwa matumizi ya muda kwa kiwango cha asilimia 15.5, kwa wasichana kutumia asilimia 16.4 na wavulana asilimia 60.9 kwa siku, huku starehe kama kuangalia luninga ikiwa ni asilimia 23,4.” Alibainisha.
Dk. Chuwa alisema mwenendo huo si wa kuridhisha chini ya kaulimbiu ya serikali ya ‘Hapa Kazi Tu’ kwa kuwa muda mwingi hutumika kwenye starehe badala ya kusoma kwa bidii na maarifa ili kuwa na taifa la kesho lenye wasomi wanaotumia teknolojia ya kisasa na kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza uchumi na hatimaye kupunguza umaskini.
Mratibu wa ILO nchi za Tanzania, Rwanda, Kenya, Uganda na Burundi, Jealous Chirove, alisema utumikishwaji wa watoto ni tatizo kwa kuwa asilimia 11 ya watoto milioni 264 wenye umri wa miaka saba hadi 17 wanatumikishwa kwenye ajira mbalimbali.
Mwakilishi wa UNICEF, Cecilia Baldesh, alisema utekelezaji wa malengo endelevu ya millennia (SDG) unataka watoto wote kupata elimu, ili ifikapo 2030 umaskini umalizike duniani, na kwamba tafiti zinaonyesha asilimia 1.8 ya watoto wanachangia kipato cha familia huku haki zao za msingi zikivunjwa.
source; IPP Media