Update:

29 July 2016

Msajili akemea Ukuta wa Chadema

Huku vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA vikiunga mkono oparesheni ya CHADEMA  ya kufanya maandamano ya mikutano ya adhara nchi nzima septemba mosi,Msajili wa vyama vya siasa jaji Francis Mutungi amekemea mpango huoJuzi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho ambayo pamoja na mambo mengine ilidhamiria kufanya operesheni waliyoipa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) ikiwa na lengo la kupaza sauti dhidi walichosema ni serikali kuiweka demokrasia vizingiti.
KAULI YA MSAJILI
Kwa upande wa Jaji Mutungi, alisema Chadema imetumia lugha ambazo ni za uchochezi na kusema kwamba, siyo mara ya kwanza kukipa onyo chama hicho kutokana na kutumia lugha za kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Alikitaka chama hicho kuacha tabia hiyo na kwamba kitaendelea kufanya hivyo kinaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema ni vizuri vyama vya siasa vikaonyesha taswira stahiki ya wanasiasa wakomavu au vyama vya siasa vya kutolea mfano ndani na nje ya mipaka ya nchi kwa kuzingatia sheria za nchi katika kuendesha shughuli zake na kuepuka vitendo, kauli na matamshi yenye lengo la kusababisha uchochezi au kufarakanisha umma na serikali yao.
“Nimepokea kwa masikitiko tamko la Chadema, la kuitangaza siku ya Septemba mosi kama siku ya mikutano ya nchi nzima kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa huku wakisema kwamba wako tayari kwa lolote lile,” alisema Jaji Mutungi.
Mtungi alisema tamko lililotolewa na Chadema limejaa lugha ya kuudhi, uchochezi, kashfa, na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Jaji Mutungi alisema kanuni ya maadili ya vyama vya siasa, tangazo la serikali namba 215 la mwaka 2017, linakataza chama cha siasa kutumia lugha ya matusi, kashfa, uongo na uchochezi na kwamba kanuni namba 5(1)(d) inakitaka kila chama cha siasa kutotoa maneno yotote au maandishi ambayo ni uongo ama kuhusu mtu yeyote au chama cha siasa chochote.
Aliongeza kuwa kanuni namba 5(1)(f) inasema kila chama cha siasa kina wajibu wa kulaani na kupinga matumizi ya lugha za matusi, vitendo vya kibabe na vurugu na matumizi ya nguvu ili kujipatia umaarufu wa chama au sababu nyingine ile.
KAULI YA CCM
Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama visisite kuchukua hatua zinaozstahili katika kukabiliana na hali hiyo
“Tunaomba vyombo vinavyohusika visisite kuchukua hatua zinazostahili bila kumuonea mtu lakini bila kufumbia macho vitendo vyenye lengo la kuwahujumu watanzania walio wengi walioamua kuchapa kazi kuitikia wito wa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya kazi,” alisema Ole Sendeka.
Sendeka aliwataka watanzania kupuuza wito wa kufanya vurugu na uvunjifu wa amani badala yake wajikite kwenye kuchapa kazi na kujitafutia maendeleo yao kwa kufanya kazi kwa bidii.
Alisema serikali haijazuia kufanyika mikutano kwenye majimbo yao na kwamba wabunge wako huru kufanya shughuli zao kwenye majimbo yao.
Aliongeza pia kuwa suala la vyama vya siasa kufanya shughuli kwa mujibu wa katiba ya vyama vyao sio jambo lililozuiliwa pia.
Kauli za vyama vya siasa
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Nassor Ahmed Mazrui, alisema CUF wanaunga mkono operesheni iliyotangazwa na Chadema kwa sababu inadai demokrasia ya wananchi.
Alisema japokuwa Chadema haikuwashirikisha katika kuunda operesheni hiyo wala hawajapewa mwaliko wowote lakini wanaunga mkono uamuzi huo.
Alisema CUF inaendeshwa kwa vikao, hivyo bado hawajakaa kujadili suala hilo lakini kimsingi kuna haja ya kuunga mkono operesheni yoyote ya kupinga ukiukwaji wa demokrasia.
“Kama watatuomba basi nasi hatutakataa, kama `solidarity’ (mshikamano) tutakaa pamoja katika kuwa `support’ (kuwaunga mkono) wenzetu,” alisema Mazrui.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alisema hawajapokea taarifa yoyote ya mwaliko kutoka Chadema kuhusu operesheni hiyo.
Alisema endapo Chadema ikiwashirikisha katika operesheni hiyo, NCCR-Mageuzi ipo tayari kuunga mkono kwa sababu ina maslahi kwa taifa.
Alipoulizwa kuhusu katazo la Rais Magufuli la kupiga marufuku mikutano ya hadhara hadi 2020, na kufanya hivyo ni kuchochea vurugu, Nyambabe alisema vyama vya upinzani haviendeshwi kwa kauli za Rais bali wanafuata katiba ya nchi inavyosema.
Alisema tamko la Rais ni kinyume cha katiba kwani vyama vya siasa kufanya mikutano ni haki yao kikatiba.