Update:

16 July 2016

Mapya yaibuka kuhusu vitambi

Tafiti mbalimbali mpya kuhusiana na viriba tumbo maarufu kama vitambi zimeibua mambo mapya ya kutisha kwa wanaume

Ni kwamba, hali hiyo ya kuwa na vitambi husababisha vifo kwa wanaume takribani mara tatu zaidi ya wanawake, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni.
Katika utafiti huo uliohusisha wanaume na wanawake karibu milioni 4 duniani kote, imebainika kuwa uwezekano wa kufa kwa wanaume kabla ya kufikisha miaka 70 ni asilimia 19 wakati kwa wanawake wenye uzito wa kawaida wastani wa kifo ukiwa ni asilimia 11.
Hata hivyo, hatari hiyo ya kifo kwa kila jinsia huwa juu zaidi na kufikia asilimia 30 kwa wanaume wenye vitambi huku kwa wanawake wenye hali hiyo ikiwa ni asilimia 15.
Kwa hesabu hizo, tafiti zimebaini kuwa hatari ya kifo kwa wanaume kabla ya kufikia umri wa miaka 70 huwa juu kwa asilimia 11 kulinganisha na wanaume wasiokuwa na vitambi huku kwa wanawake uwezekano wa kufa mapema ukiwa ni asilimia nne zaidi kwa wale wenye vitambi kulinganisha na wengine wenye uzito wa kawaida.
"Vitambi vinakamata nafasi ya pili nyuma ya uvutaji wa sigara katika kusababisha vifo vya mapema vya watu nchini Marekani," alisema kiongozi wa utafiti, Richard Peto, ambaye ni professa wa takwimu za afya katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.
"Kama mtu unaweza kupunguza uzito wako kwa takribani asilimia 10, maana yake kwa mwanamke ni sawa na kupunguza asilimia 10 ya hatari ya kufa mapema kabla ya kufikisha miaka 70 na kwa wanaume ni sawa na kupunguza uwezekano wa kufa mapema kwa asilimia 20," alisema Peto.
Hata hivyo, tafiti zilizopo hazielezi ni kwa nini wanaume wenye vitambi huwa katika hatari kubwa zaidi ya kufa mapema ywanapokuwa na vitamjbi kulinganisha na wanawake.
"Utafiti wetu haukuweza kujibu swali hilo, lakini huko nyuma iliwahi kuonekana kwamba wanume wenye vitambi wana kinga madhubuti ya insulin, kiwango cha mafuta ya ini na pia kuwa katika hatari zaidi ya kupata kisukari kulinganisha na wanawake," alisema mwandishi msaidizi wa ripoti ya utafiti huo, Dk. Emanuele Di Angelantonio, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Utafiti huo ulichapishwa kwenye mtandao Julai 13.
Mtaalamu mmoja wa Marekani alisema utafiti zaidi unahitajika ili kubaini uhusiano wa kati ya kitambi na kifo.
"Bado tuna kazi zaidi ya kufanya ili kuelewa vyema ni kwa vipi uzito kuongezeka na kupungua kwa uzito huchangia kutokea kwa vifo," alisema Barry Graubard, mtafiti mwandamizi wa takwimu za Kibaiolojia katika Taasisi ya Taifa ya Saratani nchini Marekani. Alishiriki katika kuhariri andiko la afya.
Kuepuka kitambi huwa kuna faida kadhaa zilizo wazi kwa wote, wanaume na wanawake, alisema Graubard.
"Zaidi ya yote, tunajua kwamba tafiti nyingine zimeonyesha kuwa mazoezi hupunguza hatari ya kifo kwa kila mmoja," alisema.
Katika utafiti mpya, watafiti walikusanya taarifa kutoka kwa watu wazima milioni 3.9, wenye umri wa kuanzia miaka 20 hadi 90. Taarifa hizo zimekusanywa kutoka katika tafiti 189 zilizowahi kufanyika Ulaya, Amerika ya Kaskazini na kwingineko duniani.
Wachunguzi walijumuisha taarifa za watu wote walioishi walau kwa miaka mitano. Wakati wa utafiti, takriban washiriki 400,000 walifariki.
Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa watu wenye uzito mdogo pia walikuwa katika hatari ya kufa mapema.
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) linakadiria kuwa watu wazima bilioni 1.3 duniani kote wana uzito mkubwa, na wengine milioni 600 wanakabiliwa na vitambi. Aidha, katika tafiti zilizowahi kufanyika siku za nyuma, vitambi vimekuwa vikihusishwa zaidi maradhi ya moyo, kiharusi, kisukari na kansa, watafiti walisema.
Dk. David Katz ni rais wa Chuo cha Afya na Maisha cha Marekani. Alisema: "Ingawa kwa muda mrefu kumekuwa na ushahidi wa wazi unaohusisha vitambi na kuongezeka kwa hatari ya maradhi sugu ambayo mwishowe husababisha vifo vya mapema, uhusiano wa kitambi na kifo umeibua changamoto mpya."
Utafiti huu umedhibiti changamoto nyingi zilizokwaza tafiti za awali na "kutoa matokeo ya wazi nay a uhakika zaidi –
kwamba kitambi huongeza hatari ya kutokea kwa vifo vya mapema duniani kote," alisema Katz.
Utafiti huo pia umeonyesha kwamba hatari za kifo zipo kote, kwa wenye uzito mkubwa na wenye vitambi – kadri
kitambi kinavyokuwa kikubwa, ndivyo hatari inavyoongezeka, aliongeza.
"Tatizo la vitambi linaendelea kuongezeka na hivyo kuyaweka rehani maisha ya binadamu," alisema Katz.
"Hili linasababisha kuwapo haja ya kuchukua hatua madhubuti ya kurekebisha hali hii duniani kote," aliongeza