Update:

29 July 2016

Lowassa awachongea CCM kwa Magufuli

Aliye kuwa mgombea wa urais CHADEMA kwenye uchaguzi mkuu ulio pita Edward Lowassa,Ametoa tamko kuzungumzia mwaka nje ya CCM tangu alipo hama july 28 mwaka jana huku akiwachongea wanaodaiwa kukisaliti chama na akiwataka waendelee kumpa taarifaKauli hiyo ya Lowassa inaweza kutafsiriwa kwamba inawachonganisha wanachama hao wa CCM na Mwenyekiti wao, Dk.
John Magufuli, ambaye Julai 23, mwaka huu alikabidhiwa mikoba ya uongozi wa chama hicho na orodha ya wanaodaiwa kukisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
“Nawahakikishia Watanzania na wana-Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananachi) kwa jumla, sasa hivi nina ari, nguvu na hamasa kubwa kuliko wakati mwingine wowote.
“Kwa wale wenzangu waliobaki CCM na wanaoniunga mkono, tuendelee kushikamana na kunipatia taarifa kwa hatma ya nchi yetu.
Nawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuniunga mkono mimi na wenzangu ndani Chadema,” alisema Lowassa katika tamko lake hilo.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, alisema kwa uamuzi aliouchukua wa kutoka CCM haukuwa rahisi, lakini kwa ushupavu, ujasiri na mwongozo wa Mungu, alifanikiwa kufanya hivyo.
Alisema uamuzi wake huo ni wa kihistoria katika nchi hii.
“Najivunia kwa uamuzi ule, umewafungua macho Watanzania wengi na kuimarisha demokrasia. Nimeingia Chadema nimewakuta viongozi na wanachama wenye moyo wa dhati wa kuliletea maendeleo taifa lao kivitendo. Najihisi mwenye furaha kubwa na raha kuwa katika upande huu.
“Watanzania bado wanataka mabadiliko na imezidi kuthibitisha kuwa hawawezi kuyapata ndani ya CCM. Watanzania wanataka sera na mtu mbadala wa kuongoza mabadiliko hayo. Vyote hivyo watavipata ndani ya Chadema na Ukawa kwa jumla,” alisema Lowassa.