Update:

21 July 2016

Ajiua baada ya kungundulika kuwa na VVU

Mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya Imara Security Guard, Samweli Alkado (39) amejiuwa kwa kutumia shati lake akiwa chumbani kwake mtaa wa mji wa zamani manispaa ya Mpanda mkoani Katavi baada ya kupima na kugundua kuwa ana maambukizi ya virusi vya UKIMWI


Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa mtaa huo, Magret John, tukio hilo lilitokea juzi saa 11:00 alfajiri katika mtaa aliokuwa akiishi marehemu.
Margret alisema kabla ya tukio hilo, Samwel alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mara kwa mara, hali iliyomlazimu aende Hospitali ya Wilaya kufanyiwa uchunguzi wa vipimo.
Mwenyekiti huyo wa mtaa aliwaeleza waandishi wa habari kwamba baada ya kufanyiwa uchunguzi wa vipimo, ndipo Samwel alipogundulika alikuwa akiishi na VVU.
Alisema baada ya kupatiwa majibu hayo, Samwel alianza kuchanganyikiwa, hali iliyomfanya hata utendaji wake wa kazi, kuzorota na kumfanya mwajiri wake amrejeshe kwao mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Alifafanua kuwa juzi kiongozi wa kampuni aliyokuwa akifanya kazi marehemu, Omary Ismail, alipokwenda katika nyumba aliyokuwa amepanga kwa lengo la kumpa taarifa za safari yake ya kurejea kijijini kwake.
Hata hivyo, alisema alipopiga hodi katika chumba cha Samwel, hakuitika, hivyo kumfanya aingiwe na shaka na kuwaamsha wapangaji wengine.
Alisema wapangaji wenzake pia walijaribu kubisha hodi, lakini hakuitika na ndipo viongozi wa mtaa wa Mji wa Zamani walipoamuru mlango wa chumba hicho uvunjwe.
Aliongeza kuwa baada ya kuingia ndani ya chumba, walimkuta Samwel amekufa kwa kujinyonga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kwamba polisi wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.