Update:

Mganga Mkuu afichua mbinu za kuepuka kisukari, saratani

Watanzania wameaswa kuachana na mtindo unao itwa wa kisasa wa kimaisha kama matumizi ya pombe kupita kiasi ,uvutaji wa sigara na ulaji wa vyakula vyenye mafuta ili kuepukana na maradhi yasio ambukiza kama kisukari,saratani,shinikizo la damu na moyo

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Muhammad Kambi, amefafanua kuwa elimu inapaswa kutolewa kwa jamii ili watu watambue uzito wa maradhi hayo yanayozidi kuwa tishio kwa jamii na taifa zima kwa ujumla.
Alisema maradhi hayo yamekuwa yakiongezeka kila uchao kutokana na watu kutozingatia ushauri wanaopewa na wataalamu pamoja na elimu inayotolewa kupitia vyombo vya habari na taasisi mbalimbali za kiafya nchini.
"Kama serikali, tunapambana ipasavyo kukabiliana na janga hili ikiwa ni pamoja na kuwataka watu kutembelea vituo mbalimbali vya afya ili kupima afya zao na kusisitiza walioathirika kuwahi hospitali ili kupata matibabu ya haraka," alisema Kambi.
Aidha, alisema masuala yanayoshughulikiwa na serikali katika kupambana na kasi ya maradhi hayo ni pamoja na kuongeza wataalamu wa kutibu maradhi hayo, vifaa tiba, uwepo wa dawa za kutosha pamoja na fedha za kutosha kusimamia mipango mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya utoaji huduma.
Alisisitiza jamii kutofanyia mzaha jambo hili kutokana na uzito wake na kuongeza kuwa maradhi yasiyoambukiza yanazidi kuwa tishio kubwa kwa taifa ukilinganisha na maradhi mengne hivyo kuomba elimu zaidi kutolewa kwa namna mbalimbali katika jamii ili kuokoa maisha ya wengi.

No comments