Update:

Kwa mara ya kwanza FIFA kumpata katibu mkuu mwanamke

Shirikisho la mpira wa miguu duniani (FIFA) limemteua mwanamke kwa mara ya kwanza kuwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo ambapo anaziba nafasi ya Jerome Valcke.

Fatma Samba Diouf Samoura kutoka Senegal ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu ambapo yeye ndiye mwanamke wa kwanza kuwahi kupewa wadhifa huo. Fatma Samba amezipa nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Katibu Mkuu Jerome Valcke aliyepigwa marufuku kujihusisha na masuala ya mpira wa miguu kwa miaka 12.

Fatma Samoura, 54 amekuwa akifanya kazi Umoja wa Mataifa kwa miaka 21 sasa na ataanza shuguli zake za mpira mwezi juni.

“Ni muhimu shirikisho la mpira wa miguu likazidi kuwekeza katika watu wapya katika jitihada za kuendelea kuboresha shirikisho hilo”- alisema Rais wa FIFA Gianni Infantino

“Amethibisha uwezo wake wa kuweza kujenga vilabu na kuviongoza kwa namna ambavyo inapashwa kufanyika lakini pia anaelewa kwamba suala la uwazi na uwajibika ni nguzo kwa taasisi yoyote inayofanya vizuri.”

Uteuzi wa Samoura ulitangazwa katika mkutano wa FIFA uliofanyikia Mexico ambapo umekamilisha muonekano mpya wa shirikisho hilo lililokuwa linanuka rushwa enzi za utawala wa Jerome Valcke na Rais aliyepita Sepp Blatter.

Blatter ambaye ameliongoza shirikisho hilo tangu mwaka 1998 aliondolewa mwaka jana na kuzuiwa kujihusisha na masuala yoyote ya mpira wa miguu kwa miaka 6 kufuatia kukiuka maadili ya uongozi.

Wachambuzi wa masuala ya mpira wamesema kuwa kwa shirikisho lililokuwa likinuka kila aina ya uozo kuchaguliwa kwa mwananmke katika nafasi ya juu hivyo inaonekana ni njia nzuri ya kuanza kurekebisha mambo.

Ukizingatia na masuala ya kupunguza nguvu za Rais wa FIFA, Bi. Samoura ni mtu muhimu sana. Yeye atakuwa akitekeleza majukumu ya kila siku ya FIFA kuhakikisha inafanya vizuri na kuondoa uchafu wote wa nyuma.

Ujio wa mtu mpya kutoka katika siasa za michezo utawasidia sana hasa wafuasi wa mchezo huo waliokuwa wanataka uhuru katika masuala ya mpira. Watu wamejawa na shauku ya kutaka kusikia maoni ya Bi. Samoura juu ya sakata la Qatar kuhusu kuwa mwenyeji wa kombe la Dunia mwaka 2022.

Fatma Samour alianza kufanya kazi UN akiwa kama Afisa usambazaji wa Shirika la Chakula kuanzia mwaka 1995 Roma, Italy na kuanzia hapo akawa mwakilishi wa nchi 6 za Africa moja wapo ikiwa ni Nigeria.

“Leo ni siku njema sana kwangu kwa kukabidhiwa majukumu haya” alisema Bi. Samoura.

“Hii ni nafasi sahihi kabisa sababu ya taaluma yangu, uzoefu nilionao, mbinu nilizonazo katika kujenga timu kimataifa, ambazo nitazitumia kuhakikisha mpira wa miguu unakua kote ulimwenguni.”

“FIFA inaanza kutumia mbinu mpya, na natamani sana kuwa mmoja wa watakaofanikisha mbinu hiyo kufanikiwa na ikadumu kadiri iwezekanavyo”.

No comments