Update:

Kisa cha mauaji msikiti Mwanza hiki hapa

 
Mauwaji ya watu watatu akiwemo Imamu wa msikiti wa Rahman Ibanda,Mtaa wa Mtemini, Kata ya Mkoloni, Nyamagana jijini Mwanza ,ambayo yana viashiria vya Ugaidi yalichochewa na kisasi baada ya washirika wa wauwaji hao kuwa wamekamatwa na polisi siku moja kabla

Imam huyo na wafuasi wake, waliuwawa na kundi la watu wanane waliokuwa na bunduki moja, mapanga, mashoka na majambia, kwa kuchinjwa ndani ya msikiti na watu wanaosemekana ni washirika wa Kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu (IS), ambalo linaendesha harakati zake katika nchi mbalimbali za Mashariki ya Kati.
Waliouawa katika tukio hilo ni Imamu Feruz Elias (27), mkazi wa Ibanda Relini, Mbwana Rajab (40), mkazi wa Ibanda na Khamis Mponda (28) mkazi wa Mkolani.
Habari kutoka ndani ya duru za uchunguzi mkoani Mwanza, zilizopatikana jana, zilisema polisi ilikuwa ikifuatilia mienendo ya kikundi kinachoonekana kuwa cha kigaidi na kufanikiwa kukamata wafuasi kadhaa kabla ya kutokea mauaji hayo juzi.
Uwezekano wa kuwapo kwa uhusiano baina ya wauaji hao na kikundi cha kigaidi kinachosakwa na polisi, unatokana na ukweli kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo, watu hao walihoji kuwapo kwa ibada hiyo wakati "(Waislamu) wenzetu wamekamatwa na polisi."
Imam wa msikiti na wafuasi hao katika barabara ya kwenda Shinyanga, waliuwawa wakati wa ibada ya saa 2:00 usiku na watu hao waliokuwa na bendera nyeusi yenye maandishi meupe ya Kiarabu kama bendera ya IS na pia wakiwa wameficha nyuso zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema hawezi kuliita tukio hilo la kigaidi kwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi ili kufahamu kama linahusiana na ugaidi au la.
Habari za kiuchunguzi zinadai polisi ilishtushwa na kuwapo kwa mauaji ya watu yanayodaiwa kuwa ya ujambazi, lakini bila kuwapo kwa ulazima wa majambazi kuwaua watu hao walioporwa mali zao pia.
Chanzo kimoja cha habari kutoka duru za uchunguzi kilisema kwa kawaida, jambazi huwa haui mtu kama hapakuwa na ubishi katika kusalimisha mali au fedha zinazoporwa.
Pamekuwa na matukio ya mauaji ya wafanyabiashara ya mara kwa mara, katika maduka ya simu na kutuma na kupokea fedha, ambayo yamegharimu maisha ya takriban watu wanne tangu kuanza kwa mwaka huu mkoani Mwanza.
Katika kufuatilia mauaji hayo, ndipo vyombo vya usalama vilipogundua kuwapo kwa kikundi cha kigaidi mkoani humo.
MASHUHUDA WASIMULIA
Mashuhuda walionusurika katika tukio hilo, wakizungumza na Nipashe jana eneo la msikiti huo, walisema majira ya saa 3.00 juzi usiku baada ya kumaliza swala, waliingia watu wapatao 10 wakiwa wameshika mashoka, mapanga na majambia na kuwaamuru waumini wote kulala kifudifudi.
WALIONUSURIKA
Kijana aliyenusurika katika tukio hilo, Abubakari Makabwa (19), alisema baada ya swala kumalizika, watu hao waliingia na kuwaamuru kulala chini huku wakitoa bendera nyeusi na maandishi ya meupe ya Kiarabu kisha kumtaka Imamu wa msikiti kujitokeza mbele. Bendera hiyo inafanana na ile inayotumiwa na Kundi la IS.
“Imamu alipojitokeza huku tukiwa tumelala chini, watu hao walisikika wakisema 'Kwa nini mnaswali wakati wenzetu wamekamatwa na polisi, wengine wanapigana jihad’…hali hiyo ilitushtua zaidi baada ya Imamu kuanza kuchinjwa kwa panga,” alisema Makabwa.
Alisema baada ya Imamu kukatwa kwa panga shingoni, wauaji hao walianza kuwachinja wengine waliolala kabla ya amri ya kutoka kwa mmoja wa wauaji hao, kuwaamuru watoto kuondoka ndani ya msikiti huku wakiendelea kuwachinja wengine.
Makabwa alisema baada ya kutoka akiwa anakimbia na wenzake wanne kupitia mlango wa nyuma, walikutana na mtu mwingine akiwa ameshika bunduki akilinda usalama nje, hali iliyowatia shaka zaidi.
“Tulisikia sauti ya yule mwanamke aliyekuwamo ndani akisema wapige risasi hao. Tulilala vichakani na wala hatukuonekana kutokana na wauaji hao walipofika msikitini walizima taa zote, lakini mshika bunduki hakuweza kurusha risasi yoyote,” alisema.
Aidha, alisema baada ya kufanikiwa kukimbia, watu hao walirusha bomu la mafuta ambalo lililipuka huku lingine likishindwa kulipuka ndani ya msikiti huo.
Naye manusura mwingine, Abeid Gati, alisema awali baada ya watu hao kuingia ndani ya msikiti huo, alidhani ni askari polisi hivyo kumfanya akae chini.
“Ghafla wakatuamuru kulala kifudifudi na kudai wao ni IS wamekuja kufanya kazi yao, kisha wakaanza kutushambulia na kujeruhi. Mwenzangu niliyekuwa naye pembeni alikatwa panga na kuangukia juu yangu, hali hiyo ilinifanya nionekane kama nimekufa,” alisema Gati.
Alisema baada ya tukio, alikaa kwa muda mrefu kama mfu hadi waliporusha chupa ya mlipuko na kuunguza ndoo kubwa ya plastiki na nyingine ilishindwa kulipuka, ndipo alikimbia nje kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa.
MWENYEKITI WA MTAA
Mwenyekiti wa mtaa wa Utemini, Jukaeli Kiula, alisema alipata taarifa za tukio hilo saa 3:20 usiku kutoka kwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Said, aliyekuwa mmoja wa waumini wa msikiti huo.
“Baada ya taarifa hizo, tulikusanyana kama 'wananzengo' (wanajamii) na kwenda msikiti hapo, tuliwakuta watu watatu wakiwa wamepigwa mapanga na kujeruhiwa vibaya sana, nilipiga simu polisi nao walifika eneo la tukio muda mfupi baadaye,” alisema Kiula.
Kiula alisema msikiti huo una waumini zaidi ya 20 wanaoswali hapo, hivyo baada ya kuvamiwa na watu hao walishindwa kujitetea kwa lolote kutokana na mazingira yaliyopo kwenye msikiti huo.
Katika hatua nyingine aliwaomba, wananchi wa mtaa huo kutoa ushirikiano ili watu hao waweze kupatikana kwani ni sehemu ya watu waliopokelewa na kuhifadhiwa na jamii ya eneo ulipotokea uhalifu huo.
MCHUNGA NG’OMBE
Eneo lililotokea mauaji hayo kuna misikiti miwili huku mmoja ukimilikiwa na dhehebu lililopo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na mwingine uko chini ya Aswar al Sunn.
Mchunga ng’ombe anayechunga maeneo karibu na msikiti wa Sunn, Mussa Masanja, alisema kuna eneo ambalo linamilikiwa na msikiti huo, huwa anawashuhudia vijana wakifundishwa mchezo wa ngumi na karate karibu na mlima.
“Nilikatazwa na mtu mmoja wa msikiti wa Sunn kuchungia ng’ombe kwa madai nitaharibu miti, lakini baada ya kuchungulia kwa mbali niliwaona watu wazima wawili wakiwafundisha ngumi na karate vijana hali iliyonitisha,” alisema Masanja.
MJANE WA MBWANA RAJAB
Zena Ismail ambaye kwa sasa ni mjane wa watoto watatu, wawili kati yao wasichana wa marehemu Mbwana Rajab, alisema msiba huo umemwachia simanzi kubwa pamoja na familia.
Alisema baada ya kupokea taarifa za kuuawa mume wake, hakuamini kutokana na muda mfupi nyuma aliaga kwenda msikitini kwa ajili ya swala ya usiku.
“Nashindwa kuzungumza chochote, lakini kikubwa tumepoteza baba wa familia,” alisema Zena.
KAMANDA WA POLISI
Akizungumzia tukio hilo, Msangi alisema juzi saa 2.30 usiku, katika msikiti huo, watu wasiozidi 15 wakiwa wamevalia ‘kininja’ huku wakiwa na silaha mbalimbali kama mashoka, mapanga na bendera nyeusi yenye maandishi meupe, waliingia ndani ya msikiti huo na kuzima taa.
“Watu hao walisikika wakiwaambia waumini hao, kwanini wanaswali wakati wenzao wamekamatwa na kushikiliwa na polisi, hali iliyowafanya waanze kuwashambulia papo hapo,” alisema Kamanda Msangi.
Msangi alisema watu hao waliwashambulia kwa silaha hizo watu wanne msikiti hapo na kuwajeruhi vibaya kichwani na shingoni, lakini kati yao watatu walifariki dunia na mwingine mtoto wa miaka 13, kujeruhiwa.
Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo, polisi mkoani hapa inawashikilia watu watatu huku msako mkali wa kuwasaka wengine ukiendelea maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
TAMKO LA SERIKALI
Kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge cha kujadili makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/17 bungeni mjini hapa jana asubuhi, Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema vyombo vya ulinzi na usalama vitafuatilia kwa kina chanzo cha tukio hilo.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali, kuomba mwongozo wa Spika akitaka kauli ya serikali kuhusu tukio hilo, huku akiomba lijadiliwe na Bunge zima.
"Jana (juzi) usiku mkoani Mwanza kwenye eneo linaloitwa Mkolani, kuna watu watatu waliokuwa wamevalia kininja waliingia msikitini wakati waumini wakisali na kuwakata mapanga watu watatu akiwamo imamu wa msikiti huo na watu wote watatu waliokatwa mapanga, wamefariki dunia.
"Naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika na kama unaona inafaa kwa mujibu wa Kanuni ya 47, naomba jambo hili lijadliwe ili tuone, inawezekana serikali ikatupatia majibu ya kina juu ya suala hili kwa sababu ni suala ambalo lime'create tension' kubwa hasa kwa waamini wa Kiislamu," alisema Bobali.
Akitoa mwongozo wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema tukio hilo halifanani na mazingira ya Tanzania.
"Habari ambazo ametupatia Mheshimiwa Bobali, ni za ghafla, lakini pia za kusikitisha sana," Ndugai alisema.
"Natumaini kwa niaba ya Bunge zima, tutoe salamu za rambirambi kwa wote waliopatwa na tukio hili, tuombe Mwenyezi Mungu azipokee roho zao mahali pema peponi.
"Linavyosimuliwa kama vile si tukio la Tanzania hapa. Eeh, hatuwezi kufanya mjadala kwa sababu hata tukiruhusu mjadala, tutajadili nini sasa kwa sasa hivi?
"Tuchukulie kama ni taarifa kwa serikali, acha serikali ijipange iangalie ni jambo gani linaloendelea kwa kuwa limetokea usiku wa kuamkia leo (jana), naamini kabisa vyombo vya ulinzi na usalama viko 'on', watakapokuwa tayari, watatutaarifu kuhusiana na jambo hili kadri linavyoendelea."
Baada ya maelezo hayo ya Spika, Jenista alisimama na kumpongeza Bobali kwa kulitaarifu Bunge kuhusu tukio hilo na kueleza kuwa vyombo vya dola vitalifanyia kazi.
"Kwanza nimshukuru mheshimiwa mbunge kwa taarifa hiyo. Wakati mwingine ni jambo jema Bunge hili likawa linapokea taarifa mbalimbali za matukio mbalimbali yanayotokea katika nchi yetu," alisema.
Jenista aliongeza: “Mheshimiwa Spika umetoa maelekezo na sisi, serikali tutafuatilia tuweze kujua nini kilichojiri kule na chanzo chake nini na mwongozo wa kiti chako, basi tutaona ni namna gani tunaweza tukapeana habari na kujua kabisa kwa dhati jambo gani lililotokea na hatua zilizochukuliwa."
Sourse: Nipashe