Update:

Chadema yataka Waziri ajiuzulu

Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA ) Kimemtaka waziri wa mambo ya ndani ya nchi,Charles Kitwanga,  kujiuzulu kutokana na kuhusika na mkataba wa Lugumi Enterprises Ltd na wizara yake.
Chama hicho kimesema kuwa asipojiuzulu, kitaibana serikali kwa kuanza kampeni ndani ya Bunge na kuzunguka nchi nzima.

Utekelezaji wa mkataba kati ya Kampuni ya Lugumi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, tayari unachuguzwa na Kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na matokeo yake yatawasilishwa bungeni kwa uamuzi.

Onyo hilo lilitolewa jana kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu.

Kitwanga anatuhumiwa kuwa kampuni yake ilikuwa mbia wa Lugumi Enterprises katika kutekeleza mkataba wa kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchini (AFIS).

Mwalimu alisema pia Chadema imeagiza hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Msemaji wa Upinzani kwenye wizara hiyo, Godbless Lema, iliyokataliwa na Bunge, sasa isambazwe kwenye matawi yote ya chama hicho na mitandao yote ya kijamii na kwamba Bunge isichukulie suala hilo ni jepesi.

“Sisi tunaunga mkono hotuba hii na Chama kimetoa maelekezo na tumewapa kazi Baraza la Vijana wetu kuisambaza nchi nzima kupitia ofisi zetu na mitandao yetu ya kijamii ili watu waone ubaya huo unaosemwa, halafu wananchi ndiyo watuhukumu,” alisema.

“Sisi siyo wa kuhukumiwa na Chama Cha Mapinduzi... wananchi ndiyo watuhukumu,” aliongeza Mwalimu.