Update:

Wabelgiji wachemsha jina la Samatta, kocha wake afunguka
SAA 24 kabla sijaondoka Jiji la Genk Napata bahati ya kufanya majumuisho ya matembezi yangu kwa Samatta kwa kutazama pambano lao la mwisho la msimu kabla ya kuanza mechi za mtoano baada ya mechi za kimataifa. Wanacheza na Oostende.

Ni mechi ambayo Samatta anaanza kwa mara ya kwanza baada ya kocha kuamua kumweka nje nyota wa kimataifa wa Ugiriki, Nikolas Krelis. Samatta anatakiwa kuwa na kazi kubwa ya kumshawishi kocha wake, Peter Maes kwamba yeye anastahili kuanza kuliko Mgiriki wake.

Oostende inajumuisha mastaa kama staa wa Afrika Kusini, Andile Jali, mlinzi wa kushoto ni mdogo wake Romelu Lukaku, Jordan Lukaku ambaye pia anakipiga timu ya taifa ya Ubelgiji. Kiungo kuna staa wa Zimbabwe, Knowledge Musona. Mlinzi wa kati ambaye alikuwa anamkaba Samatta ni David Rozenhal, nyota wa zamani wa Newcastle ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Czech.

Kabla mechi haijaanza napata nafasi ya kuongea na waandishi wa Genk kuhusu masuala mbalimbali yanayoizunguka timu yao. Wanapomzungumzia Samatta nashangaa kusikia wanamwita kwa jina la Ally. Naam, nafahamu jina la Samatta ni Mbwana Ally Samatta, lakini sijui kwa nini wamelichagua jina la Ally. Hata nyumbani kwake, mtumishi wake wa ndani wa kizungu Mishka huwa anamwita Samatta jina la Ally tu. Wakati mtangazaji anapoanza kutangaza vikosi vya timu zote mbili anatumia jina moja tu la kwanza kwa wachezaji wote wa nyumbani halafu mashabiki wanamalizia. Inapofika zamu ya Samatta mtangazaji anasema “Ally”, mashabiki wanaitikia ‘Samatta’

Samatta anafunga bao katika dakika ya 23 na anaonekana kuwa kipenzi cha mashabiki. Mtangazaji anarudia kusema tena vile vile akianzia na jina la Ally na mashabiki wanaitikia Samatta. Baada ya hapo mechi inaendelea lakini nakuwa na kinyongo sana. Kwa nini mawinga wa Genk hawamlishi mipira Samatta? Kila wakipata hawapigi krosi, wanajaribu kuingia nayo ndani. Wanapoteza. Krosi moja nzuri ambayo winga wa kushoto Mjamaica, Leon Balley alipiga ndiyo ambayo Samatta alifunga. Kwa nini hawafanyi hivyo tena na tena?

Mwisho wa mechi nakuwa na maswali mawili ya kumuuliza Samatta. Kwanza ni kwa nini anaitwa Ally na pili ni kwa nini jamaa hawampasii sana kutoka pembeni na hata katikati. Kama wangefanya hivyo kwa kasi ya hisia zangu. Samatta ninayemfahamu angefunga zaidi ya bao moja.

“Brother huku jina la Mbwana unadhani wanaanzaje kulitamka? Hawawezi hawa jamaa. Wameamua kuchukua jina la Ally tu kwa sababu ni rahisi pamoja na la Samatta. Halafu si unajua huku kuna kina Ally wapo. Wanatoka nchi za Kiafrika za Waarabu kwa hiyo hawaoni tatizo kutamka Ally,” anasema Samatta.

Hata hivyo, hapo hapo Samatta ananijibu swali langu jingine ambalo lilinifanya niondoke uwanjani na hasira licha ya Samatta kufunga bao moja. Kwa nini mawinga wake hawapigi pasi?

“Yaani jamaa ndio walivyo. Genk tunacheza mpira mgumu sana tukifika mbele. Kuna mtu nilimuuliza akaniambia Ligi ya hapa wachezaji wanapenda sana kuonyesha uwezo wao binafsi kwa ajili ya kujiuza kwa sababu mawakala wanatazama sana Ligi ya hapa,” anasema Samatta.

“Hata yule mshambuliaji mwenzangu (Nikos Krelis) naye akicheza naona inakuwa hivyo hivyo. Siyo kwamba walikuwa wananinyima mimi tu. Huku jamaa ndivyo walivyo. Kila mtu anaweza mpira chini anakokota tu,” anasema Samatta.

Ni kweli. Baada ya mechi, Samatta anaonekana kuwa rafiki wa karibu sana na winga wa kimataifa wa Jamaica, Leon Bailey ambaye licha ya kupiga krosi ambayo Samatta alifunga, lakini bado angeweza kupiga krosi nyingi kwa Samatta.

Bailey na Samatta wanasubiriwa kwa hamu katika eneo la kuongea na waandishi wa habari baada ya mechi (Mixed Zone) na wanaonekana kuongea kwa furaha sana na waandishi wa habari hasa baada ya timu yao kushinda mabao 4-1 mechi hiyo. Bailey ndiye aliyefunga bao la pili baada ya Samatta kufunga la kwanza.

No comments