Update:

Rais Magufuli asamehe wafungwa 580, awapunguzia kifungo 2,971

Kufuatia msamaha huo, wafungwa 580 wameachiwa huru, huku wengine 2,971 wakiendelea kubaki gerezani kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habarina na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jana na kutiwa saini na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira, Rais Magufuli ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa hiyo ilisema wafungwa waliopatiwa msamaha huo ni pamoja na wagonjwa wa ukimwi, kifua kikuu (TB) na saratani waliothibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

Wengine ni wafungwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70, wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Pia wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili ambao ulemavu wao umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu mkoa au wilaya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, kifungo cha maisha gerezani, unyang’anyi, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya na makosa ya rushwa.

Aidha, hautawahusu wafungwa waliopatikana na silaha , risasi au milipuko isivyo halali, shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa kama hayo.

No comments