Update:

Bashe aanika madudu elimu, ataka tume ya Rais kuchunguzeMaelezo hayo ya Bashe yamo kwenye hoja binafsi anayotarajia kuiwasilisha bungeni ambayo kwa sasa iko katika ngazi ya chama kabla ya kuwasilishwa kwenye Ofisi ya Spika.

Hoja hiyo ambayo gazeti hili imeiona, inasema madudu yaliyo kwenye mfumo wa elimu, ndiyo yamesababisha elimu kushuka kila uchao huku elimu itolewayo nchini ikiibua matabaka ya wenye nacho na wasio nacho.

Katika hoja yake hiyo, Bashe anasema mfumo wa elimu kwa muda mrefu umeonyesha udhaifu katika usimamizi, uendeshaji, udhibiti na ugharimiaji tangu taifa lilipoamua kufanya ugatuzi wa madaraka, uliosababisha sekta ya elimu kuendeshwa chini ya wizara tatu tofauti.

“Wizara inayoshughulikia elimu imeachiwa sera pekee, wakati ajira za waalimu zinasimamiwa na wizara inayoshughulikia utumishi na wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa.

“Mfumo huu umetuletea matokeo yasiyoridhisha. Kwa mfano, waziri wa elimu, hana mamlaka juu ya nidhamu, maslahi, mafunzo na usimamizi wa mwalimu aliyeko Nzega na majimbo mengine,” anasema Bashe kwenye hoja yake hiyo.

Wakati serikali imekuja na mfumo wa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, Bashe anasema: “Kwa sasa elimu mpaka kidato cha nne hutolewa bure lakini elimu bora inauzwa.”

Anasema imebainika kwamba Tanzania ina mfumo wa elimu usiojali usawa kwa kiwango cha juu, mfumo kwa ajili ya makundi mawili, moja la matajiri na lingine la masikini huku akibainisha kwamba mfumo wa elimu ya shule bora za umma ni kwa ajili ya watu wa kada ya kati.

Katika hoja yake hiyo, anasema asilimia 16 pekee ya bajeti ya sekta ya elimu hutengwa kwa ajili ya kugharimia maendeleo wakati taasisi na wakala 88 zinatafuna asilimia 84 ya bajeti nzima ya sekta ya elimu ambayo ni wastani wa Sh. trilioni 3.88.

Kwa mujibu wa Bashe, kwa sasa shule za msingi na sekondari hazikaguliwi kwa kiwango cha kuridhisha kwa kuwa asilimia 9.1 ya shule za msingi na asilimia 21.4 ya shule za sekondari ndizo hukaguliwa kwa mwaka.
Alisema ugharimiaji hafifu wa sekta ya elimu umedumaza kiwango cha watoto kujifunza darasani kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Pia alisema utafiti unaonyesha uwezo wa watoto kujifunza kusoma na kuhesabu ni mdogo kwa sababu inakadiriwa kuwa asilimia 45 pekee ya watoto wa darasa la tatu wanaweza kusoma kwa ufasaha hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili.

Alisema ni asilimia 19 pekee ya watoto hao hao wa darasa la tatu wanaweza kusoma kwa ufasaha hadithi ya kingereza ya darasa la pili.

Kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika elimu umepoteza mwelekeo kuhusu ugharimiaji wa sekta ya elimu na kwamba kuna upungufu wa ugharimiaji wa elimu ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano unapendekeza ugharimiaji wa elimu ya misingi uwe Sh. trilioni 1.35 ambazo ni sawa na asilimia 28 ya fedha zote zinazotarajiwa kutengwa kwa miaka yote mitano (Sh. trilioni 4.89).” alisema.

Alisema elimu ya msingi imetengewa bajeti finyu ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17 kwa kpewa Sh. bilioni 156.73 sawa na asilimia 17 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ya Wizara Elimu, Sanyansi, Teknolojia na Ufundi katika mwaka wa fedha 2016/17.

“Mpango wa Maendeleo ya “elimu bure” katika shule za sekondari umetengewa asilimia nne tu ya fedha zote katika miaka mitano ijayo. Hakuna uhalisia katika ugharimiaji wa mpango wa elimu bure nchini kwa shule za sekondari,” alisema Bashe.

Alisema wakati sekta nzima ya elimu ikisimamiwa na zaidi ya wizara moja, matumizi ya kawaida ya Wizaraya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, yanakisiwa kuwa Sh. bilioni 499.2, kwa mantiki hiyo, hakuna uhalisia katika matumizi ya kawaida ya sekta hiyo.

No comments