Update:

Adson Kagiye:"Niwakati wa mabadiliko"


Siku moja niliisikia hadithi ambayo ilinishangaza sana kutokana na kitu nilichojifunza kutokana na hadithi hiyo.Ilikuwa ni kuhusu mtu mmoja mlevi ambaye kila wakati alipokuwa anarudi nyumbani akiwa amelewa alikuwa anakutana na mbwa anayebweka,mkali sana na anamkimbiza na mlevi yule hukimbia.Mbwa huyu aliendelea kufanya hivi kila siku wakati mlevi huyu alipokuwa anapita katika maeneo yale.

Siku moja yule mlevi akajisemea moyoni-“Hivi nitakuwa mtumwa wa kumkimbia mbwa huyu hadi lini?” akaamua siku hiyo atafute fimbo kubwa ili wakati anarudi akikutana na mbwa yule badala ya kumkimbia aweze kumkabili.Alipofika karibu na mbwa,kama ilivyo ada mbwa alijua atamkimbia lakini yule mlevi alichukua fimbo yake na akaanza kumsogelea.Kadiri alivyomsogelea ndivyo mbwa alivyozidi kusogea nyuma,na mlevi alipomwangalia kwa makini akagundua kuwa kumbe mbwa yule hana meno kabisa(Kibogoyo)—Amekuwa akimkimbia mbwa asiye na meno kwa miaka mingi.Alipogundua hilo akapata ujasiri zaidi na akaanza kumkimbiza mbwa na tangu siku hiyo utumwa na hofu yake ikaisha.

Ndivyo ilivyo katika maisha,matatizo mengi tunayoyaogopa na kuyakimbia sio makubwa au magumu kama tunavyofikiria.Siku tutakapoamua kuyakabili tutashangaa jinsi ambavyo ni marahisi kuyatatua.Kuna mambo mawili muhimu ya Kujifunza leo:

1)Fanya Maamuzi thabiti ya Kukabiliana na Changamoto Yako:
Bila Kujali tatizo unalokabiliana nalo limedumu kwa muda gani katika maisha yako,bila kujali wangapi walishidwa katika kulitatua;unachotakiwa kujua ni kuwa kila tatizo lina majibu yake kama ukiamua kulikabili kwa dhati.

Jambo la muhimu ni kuwa,usiruhusu kumlaumu mtu kwa tatizo lako,chukua jukumu la kupata ufumbuzi bila kujali kama kuna mtu alikusababishia ama la.Bila kujali mbwa(tatizo) amekuwa akikubwekea(likikusumbua) miaka mingapi,amua kutengeneza ukurasa mpya katika maisha yako.

Jisemee mwenyewe-“Kuanzia leo,tatizo hili halitaendelea kunikosesha furaha na kunikosesha ujasiri,nitalikabili na nitalishinda”.Hongera,huo ndio mwanzo wa kulitatua tatizo husika!

2)Chukua Hatua Mara Moja:
Mara baada ya Kufanya maamuzi thabiti ya kukabiliana na changamoto yako inayokukabili,usichelewe,anza mara moja kuchukua hatua kuelekea ushindi wako.

Kama umeshaamua kuwa aliyekuumiza kwa kukusaliti na kukuacha bila kosa umeshamsamehe na utaanza maisha mapya,jikung’ute mavumbi ya machozi na maumivu,mtangazie msamaha na anza maisha mapya.Kama uliapply kazi mara nyingi na haukupata,jipe nguvu mpya na anza kuapply kwa kasi mpya,Kama ulifukuzwa kazi kwa kusingiziwa,usiendelee
kulalamika anza hatua nyingine,kama ulitafuta mtaji kwa muda mrefu na haukupata,basi tafuta tena leo---jiambie kuwa changamoto hizo zote ni mbwa asiye na meno.Chukua hatua kufanya jambo leo.

Ili ufanikiwe,usifanye kosa la kusubiri kesho.Kwa jambo lolote lile unalotaka kuchukua hatua.Anza leo,Anza Mara Moja.Utakapoanza utagundua kuwa matatizo mengi uliyonayo sio magumu kama unavyofikiria,ukianza kuyakabili utashangaa utakavyofanikiwa.
Ndoto Yako Inawezekana,timiza wajibu wako!!

����Adson J. Kagiye����
0756508071

No comments