Update:

Unajenga uchumi wa aina gani mwaka huu?


ILIPATA kunenwa na wazee wa zamani kwamba hapo zamani za kale kulikuwa na kijiji kimoja ambacho waliishi watu wenye uwezo lakini walikuwa na shida ya maji. Mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na kamati yake wakatangaza tenda kwa mtu ambaye angeweza kuwa anawaletea maji hapo kijijini ili kwamba serikari ya kijiji iwe inamlipa. Wakajitokeza watu wawili kuomba hiyo kazi ya kuleta maji hapo kijijini. Watu hao wawili wote walipata hiyo tenda kwasababu uhitaji wa maji hapo kijijini ulikuwa mkubwa.
Wakasaini mikataba na viongozi wa kijiji ili kuweka utaratibu mzuri.
Viongozi wa kijiji walijenga matenki mawili makubwa ya kuhifadhia maji, kwa hiyo ikaamuriwa kuwa hao waleta maji kijijini watakuwa wakileta maji yao na kuyaweka kwenye matenki hayo na kisha kila baada ya wiki watakuwa wakilipwa fedha zao kwa kiwango cha maji walicholeta.
Baada ya hapo hawa jamaa waliondoka kila mtu kwake kujipanga. Baada ya siku mbili mmoja kati ya wale waliopewa tenda alienda sokoni akanunua madumi 10 ya plastiki ya lita 20 kwa kila moja, akawa anasafiri kwa treni kuelekea mjini na kisha anachota maji masafi kwenye mto mkubwa na kuyaleta pale kijijini. Alianza kuleta maji pale kijijini kwa bidii na akaanza kulipwa pesa yake. Wananchi walifurahi kwa uchapakazi wake na ubunifu.
Mazingira ya kijiji hicho
Kijijini hapo kilikuwa na reli ambapo kila siku treni ilikuwa ikipita kwenda mjini, na kurudi siku ya pili yake. Kwa hiyo yule bwana alikuwa akitumia usafiri wa treni kuleta maji pale kijijini.
Mleta maji wa pili
Huyu jamaa yeye alikwenda benki akaonyesha mkataba wa tenda ya kupeleka maji pale kijijini, kisha akaomba mkopo wa kujenga miundo mbinu ya maji kutoka pale mtoni mpaka pale kijijini. Yule bwana baada ya kupewa fedha, akaajiri mafundi bomba, kisha wakachimba bomba la maji kutoka pale mtoni alikokuwa akichota maji yule bwana wa treni mpaka pale kijijini. Alipokwisha kufunga mabomba ya maji aliajiri wasimamizi wa huo mradi wa maji. Baadaye vijiji vingine vilivyokuwa na tatizo la maji viliomba kuunganishiwa maji pia, jamaa akaviunganishia maji. Baadaye tena wanavijiji wakaomba kuunganishiwa maji katika nyumba zao za kuishi, jamaa akawaunganishia. Biashara yake ikapanuka na kuleta manufaa kwa watu wengi.
1. Je wadhani watu hawa wawili wanatofautiana? Kama jibu ni ndiyo, tofauti zao ni nini?
2. Je ili mtu awe na Mawazo kama ya huyu jamaa wa pili, anatakiwa afanye nini?
3. Je hali ya kubuni na kuendesha biashara kwa mtindo wa huyu jamaa wa kwanza(mbeba madumu) inasababishwa na nini?
4. Je unadhani hali ya sasa ya maendeleo ya kiuchumi duniani inahitaji watu wa aina gani? Je ni wa aina ya Jamaa wa kwanza(mbeba madumu) au jamaa wa pili?
5. Je unafikiri yule bwana aliyekuwa akichota maji kwa madumu mtoni alifanyaje baada ya mwenzake kuweka mabomba ya maji pale kijijini na katika kila nyumba?
6. Je wewe binafsi kama unafanya biashara, unafanya biashara kwa kumfanania nani kati ya hawa jamaa wawili? Na ungependa kufanya biashara kwa kumfanania nani?
Source: Professor Joseph Mayagila 

No comments