Update:

Vijana toka JKT kupata Ajira Dar


Halmashauri ya Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam imejipanga kuajiri vijana waliopita Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kama mgambo ikiwa ni jitihada za Halmashauri hiyo kupambana na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya kazi hiyo kwa baadhi ya mgambo kujihusisha na vitendo vya rushwa.


Hayo yamesemwa leo na Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala Bi.Tabu Shahibu wakati akitoa ufafanuzi kwa njia ya simu kuhusu malalamiko ya wananchi yanayohusu mgambo wa Halmashauri hiyo kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wakitimiza majukumu yao.


“Tumeona tuanze kuajiri vijana waliopata mafunzo kupitia JKT ili kuondokana na malalamiko ya rushwa kutoka kwa baadhi ya mgambo wanaofanya kazi hiyo katika Halmashauri ya yetu,tunaamini vijana hao wamefundishwa maadili ya utumishi na uzalendo,


“Nasisitiza askari mgambo yoyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa tutamchukulia hatua kwa kukatisha mkataba wake wa kazi na atachukuliwa hatua za kisheria Alisema Tabu.


Bi. Tabu aliwataka wananchi watoe taarifa za askari mgambo yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa ili kufanikisha wamewaondoa na kurudisha imani ya wananchi kwa Jeshi la mgambo nchini.


Aidha, Bi. Tabu amewaonya mgambo waliomaliza mkataba ama kufukuzwa kazi kutotumia vitambulisho feki kufanya kazi za mgambo na kujihusisha na vitendo vya rushwa katika manispaa yake la sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria na atakayekamatwa atafikishwa mahakamani kwa kosa la kutumia kitambulisho ambacho siyo halali kinyume cha sheria.


Mgambo wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa katika Manispaa mbalimbali nchini hali inayosababisha usubufu kero kwa wananchi na Serikali kupoteza mapato yake kwani fedha nyingi huishia mikononi mwa watu ambao sio waaminifu.

No comments