Update:

02 February 2016

MPANGO WA TASAF AWAMU YA TATU KUBORESHWA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Angella Kairuki akijibu maswali toka kwa wabunge katika kikao cha 6 cha Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma.SERIKALI imejipanga kuborsha zaidi mpango wa kunusuru Kaya masikini nchi ujulikanao kama TASAF kwa awamu ya tatu kwa kutengeneza miundombinu mizuri ya kutambua Kaya zinazolengwa na kuondoa malalamiko ya wananchi kuwa mpango huu umekuwa ni wa Kaya chache na fedha hizo utolewa kwa upendeleo.
Akijibu swali la Mhe.Magdalena Hamisi Sakaya Mbunge wa Kaliua (CUF) lililouliza ni vigezo gani vinatumika kuondoa Kaya zilizopendekezwa kwenye mradi na kubakiza Kaya chache, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki amesema mpango wa kunusuru Kaya maskini hutambulishwa kijijini na wataalam kutoka Halmashauri husika kwa kusimamiwa na uongozi wa kijiji kisha kuweka vigezo vya Kaya maskini.
“ Wakusanya taarifa huchaguliwa kutoka miongoni mwa vijana wanaoishi kijijini hapo na kupitia nyumba kwa nyumba kuorodhesha Kaya ambazo zinakidhi vigezo vilivyoanishwa na mkutano wa Kijiji ila bado kuna malalamiko yanayotolewa kuwa Kaya maskini zinaachwa na kupewa Kaya nyingine ambazo sio maskini kwa kuliona tatizo hilo suala hili tunalifanyia uchunguzi na tunaomba watu watoe taarifa ikiwa wataona ukiukwaji wa uorodheshaji wa Kaya zitakazohusika na mpango huu ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya yoyote atakaye bainika kufanya hivyo”
“ Mpaka sasa kutokana malalamiko yaliyojitokeza katika kuorodhesha Kaya maskini zinazotakiwa kuwezeshwa na mpango huu tumewaajibisha watendaji toka Wilaya za Karagwe, Kagera na Kibondo, Kigoma na tuomba kupewa taarifa kwa sehemu yoyote ambapo kutatokea tatizo kama hili na tutachukua hatua mara moja kuokoa fedha zilizotakiwa kwenda kusaidia watu husika” Alisema Mhe Angella Kairuki.
Aidha Mhe. Angella Kairuki ameongeza kuwa kuna taarifa zinazoenezwa kuwa fedha za mpango wa TASAF Awamu ya Tatu ni fedha za freemasons, taarifa hizo sio za kweli kwani fedha hizi zizantolewa na Serikali ili kusaidia Kaya maskini ili ziweze kujikwamua kiuchumi kwa kuweza kupata Elimu Malazi na chakula bora.
TASAF ni mpango wa kunusuru Kaya maskini na imekuwa katika awamu tatu mpaka hadi sasa kwa ajili ya kuwezesha Kaya maskini kujikwamua kiuchumi.