Update:

Mke wa Rais ataka matatizo ya wazee, walemavu kushughulikiwa.

 
Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli.
Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli, ameziomba taasisi za serikali na binafsi kushirikiana katika kutatua changamoto zinazovikabili vituo 17 vya makazi ya wazee na walemavu wasiojiweza.
 
Wito huo aliutoa jana alipotembelea Makazi ya Wazee na Watu wenye Walemavu wasiojiweza cha Nunge, Kigamboni jijini Dar es Salaam ambapo alitumia fursa hiyo kuwakabidhi zawadi.
 
Zawadi alizozitoa ni mchele kilo 3,000, unga kilo 3,000 na maharage kilo 1,200. Alisema kulingana na idadi ya watu hao kila mmoja atapewa kilo 25 za mchele, kilo 25 za unga na kilo 10 za maharage.
 
“Natambua zawadi tuliyoileta ni ndogo na haiwezi kumaliza matatizo yote mliyo nayo, lakini ni matumaini yangu kuwa zawadi hii inaweza kuwa chachu ya kuamsha hamasa ya kwa watu na vikundi vingine kujitoa kusaidia watu wasiojiweza,” alisema. 
 
Katika hotuba yake, Mama Janeth aliahidi kushirikiana na wadau wote ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili watu wa kituo hicho.
 
“Napenda kuchukua nafasi hii kuziomba na kuzihamasisha taasisi za serikali na zisizo za serikali kushirikiana katika kutatua changamoto zinazokabili kituo hiki na vingine vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema.
 
Alisema amefarijika kwa sababu miongoni mwa wageni aliokuwa nao ni viongozi wa serikali, ambao watazichukua changamoto hizo ikiwamo ya  uvamizi wa eneo la kituo.
 
Alisema endapo watu wote watajitoa kwa dhati kuwahudumia wazee na watu wasiojiweza, hali hiyo itasadia  kuwapunguzia makali ya maisha.
 
Mama Janeth aliwasilisha salamu za Rais Dk. John Magufuli kwa wazee hao na kuwaeleza kuwa yuko pamoja nao na kwamba serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wazee na watu wasiojiweza wanapata huduma zote muhimu kwa kadri ya uwezo wake.
 
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazothamini na kuwaheshimu wazee na watu wasiojiweza hivyo imeweza kupitisha sera na miongozo mbalimbali ili kuwalinda na kuwatetea.