Update:

Matokeo kidato cha nne: Mazito yaibuka.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde.
Baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), wiki iliyopita kutangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba, mwaka jana, baadhi ya wadau wamekuwa na maoni tofauti.
 
Baadhi ya wadau hao wamesema matokeo hayo ni janga na yatafanya shule binafsi kukosa wanafunzi wa kidato cha tano na hatimaye vyuo vikuu kuu navyo kukumbwa na uhaba huo.
 
Katika matokeo ya mtihani huo, wanafunzi waliofaulu kwa kupata daraja la kwanza mpaka la tatu ni 89,929 sawa na asilimia 25.34 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo.
 
Wadau hao walisema baadhi ya wanafunzi kwenye kundi hili, pia hawatapata nafasi ya kujiunga na kidato cha tano kutokana na alama za ufaulu kwenye mchepuo wanaotaka kutoendana.
 
NECTA 
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema: "Ukisema ubora wa ufaulu sisi tunahangaika na madaraja matatu, la  kwanza mpaka la tatu, na ukiangalia takwimu kwenye haya madaraja, waliofaulu ni wengi kuliko mwaka jana (2014).
 
“Lakini ni asilimia 25, ukipata watu wa daraja la kwanza mpaka la tatu asilimia 25, tafsiri ya jumla ni kwamba ni robo ya watu 433,000, ambao ndio wamefaulu vizuri.
 
"Tunasema wamefaulu vizuri kwa sababu hao ndio wadahiliwa wa kidato cha tano, kama huu ungekuwa mthani wa kidato cha sita tungesema hawa ndio wadahiliwa wa chuo kikuu,” alisema.
 
Dk. Msonde alisema wakati watahiniwa wanaoweza kuchaguliwa kuingia kidato cha tano wakiwa takriban 80,000, malengo ya nchi ni kuhakikisha wanafunzi 200,000 wanapata sifa za kujiunga na vyuo vikuu.
 
“Sasa kama leo tuna robo tu ndio wanaweza kudahiliwa kwenda kidato cha tano, ambao hao si wote watakaokwenda chuo kikuu, ndiyo kusema kama watu 80,000 au 70,000 (wataingia kidato cha tano) maana hapa 89,929 (waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu). Kumbuka  wako ambao 'combination' hazijakubali (masomo kwa michepuo), kwa hiyo unaweza kuwa na watu 60,000 watakaoenda chuo kikuu.
 
“Sasa kama unapeleka watu 60,000 kidato cha tano, yawezekana ukapata 40,000 kwenda chuo kikuu, kumbuka sasa hivi tunavyozungumza vyuo vikuu kuna nafasi 80,000 kila mwaka zinatakiwa kujazwa.
 
"Kwa idadi hii kwa wanaopata daraja la kwanza mpaka la tatu bado tuna kazi, kwa sababu ili tuwe pazuri tunahitaji hii asilimia 25 ya daraja la kwanza mpaka la tatu, tuipandishe ifike asilimia 50,” alisema Dk. Msonde.
 
Alisema kwa idadi ya wanafunzi wanaopata daraja la kwanza mpaka la tatu kwa sasa, nafasi za vyuo vikuu zilizo wazi haziwezi kujazwa.
 
Alisema mwaka jana kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita waliokuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu ni 38,000 kati ya mahitaji ambayo ni 80,000.
 
“Kama mkakati ni kutaka vyuo vikuu vipate watu walio bora 80,000 lazima tuanzie chini. Lazima tupande kwa daraja la kwanza mpaka la tatu kufikia asilimia 50.
 
"Ili ufike huko, lazima tuangalie ufaulu wa masomo. Sasa hivi tunasema ufaulu wa masomo umepanda ni sawa, lakini masomo yaliyo mengi ufaulu uko chini ya wastani,” alisema Dk. Msonde.
 
Ufaulu wa kila somo kwa mwaka 2014 na 2015 na asilimia zake kwenye mabano ni kama ifuatavyo, Elimu ya uraia (Civics) mwaka 2014 (37.70) mwaka 2015 (50.56), Historia mwaka 2014 (37.41) mwaka 2015 (47.60), Jografia mwaka 2014  (37.96)  mwaka 2015 (48.70), Kiswahili mwaka 2014 (69.66) na mwaka 2015 (77.63).
 
Kingereza mwaka 2014(55.10) mwaka 2015 (56.19), Fizikia mwaka 2014 (46.71) mwaka 2015 (44.30), Kemia mwaka 2014 (56.73) mwaka 2015 (60.11), Baiolojia mwaka 2014 ilikuwa (48.30) mwaka 2015 (53.74), Hisabati mwaka 2014 (19.58) mwaka 2015 (16.76), Biashara mwaka 2014 (34.29) mwaka 2015 (36.08) na Bookeeping mwaka 2014 (42.20) mwaka 2015 (43.48).
 
Akifafanua kuhusu ufaulu huo, Dk. Msonde alisema: “Hata nikisema Historia wamepanda kutoka asilimia 37.41 mwaka 2014 mpaka 47.60,  ina maana zaidi ya asilimia 50 ya  wanafunzi wameshindwa historia.
 
"Kushindwa maana yake wameshindwa kupata D, yaani wameshindwa kupata alama 30, zaidi ya wanafunzi 230,000 wameshindwa kupata alama 30, maana ufaulu ni nikisema wameshindwa inamaana wote wana F (F=0-29).
 
"Sasa lazima tuwe na mkakati wa darasani wa kuhakikisha kila mwanafunzi anapata wastani wa chini wa kila somo (30), huo ndio uwe mkakati wa darasani. Kama mwalimu anaaingia darasani kufundisha ajue huo ndio mkakati. Wote wakiweka mkakati huo madaraja haya yatapanda.”
 
Akizungumzia kukariri darasa kwa wanafunzi ambao hawajafikia wastani, mbinu iliyokuwa ikitumiwa zaidi na shule binafsi, alisema kwa sasa kitu hicho hakipo.
 
“Sasa hivi watoto wakishaingia kidato cha kwanza ndio watahiniwa wangu wa kidato cha pili hata usiposajili, nitakuletea tu nikwambie fulani na fulani wako wapi.
 
"Sasa hivi mtihani wa kuchuja ni wa taifa, kidato cha pili ndiyo utamchuja akifika hapo ni kidato cha nne, mimi naamini mwalimu mzuri ni yule anayebadilisha kitu kibaya kiwe kizuri,” alisema.
 
Alisema baadhi ya shule walitumia vibaya mtindo huo na kuumiza wazazi waliokuwa wanalazimika kulipa gharama kubwa ya ada kwa mwanafunzi kukariri darasa kwa kushindwa kufikisha wastani ambao labda ulikuwa 40 au 60 huku wengine wakiacha shule kwa wazazi wao kushindwa kugharamia.
 
Alisema kwa sasa mtoto anakariri darasa kwa kibali maalumu cha Kamishna wa Elimu pekee.
 
TCU
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Prof. Yunus Mgaya akizungumza suala hilo, alisema ni kweli ubora wa ufaulu umepungua, jambo ambalo litaendelea kuathiri vyuo vikuu nchini.
 
“Mahitaji ya vyuo vikuu na vingine vinavyotoa shahada kama IFM (Chuo cha Usimamizi wa Fedha), CBE (Chuo cha Elimu ya Biashara), mahitaji yetu ni wanafunzi 100,000 ukitaka ujaze nafasi za shahada zinazotolewa na vyuo hivi.
 
"Ukipata hao kila chuo kitakuwa na wanafunzi wa kutosha. Mwaka jana tumepeleka vijana tukabaki na mapengo kama 35,000 kwa sababu jumla tulipeleka 65,000 na mahitaji yalikuwa ndiyo hiyo 100,000. Kwa hiyo 35,000 ni pengo ambalo halijajazwa na kwa mfumo ulivyo labda tuuongeza shule za kidato cha tano na sita vinginevyo pengo litaendelea kuwapo,” alisema Prof. Mgaya.
 
Alipoulizwa juu ya shule zinazofungwa kwa kukosa wanafunzi,  Prof. Mgaya alisema nyingi ni zile za binafsi ambazo baadhi yake, wazazi wanashindwa kugharamia ada.
 
“Mwaka jana wanafunzi 17,000 wa kidato cha nne walifaulu kwenda kidato cha tano, lakini walishindwa kwenda kwa sababu shule za serikali zimejaa na wazazi hawakuweza kuwapelaka shule binafsi. Kwa hiyo kuna shida, Tanzania lazima tubadilike.
 
"Tanzania leo tuko chini kwenye idadi ya watu wenye umri wa kwenda vyuo vikuu, ambao wanaenda ni asilimia tatu wakati huko Ulaya wanaoenda ni mpaka asilimia 60, hivyo lazima turekebisho hayo maeneo kwa sababu hatuna wataalam wa kutosha,” alisema.
    
PROF. NDALICHAKO
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, alisema licha ya ufaulu kwa matokeo ya mwaka 2015 kuonekana umepungua kulinganisha na ule wa 2014, idadi ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu umeongezeka kwa watu 6,000 kwa sababu watahiniwa wa mwaka jana walikuwa wengi zaidi. 
 
“Asilimia imepungua lakini ukiangalia waliofanya mtihani mwaka jana na mwaka huu ni tofauti, mwaka 2015, watahiniwa wa shule walikuwa takriban 394,000 wakati mwaka 2014, watahiniwa wa shule walikuwa 244,000 kwa hiyo hapa kuna ongezeko la karibu wanafunzi 150,000.
 
“Ukiangalia waliopata daraja la kwanza wameongezeka watoto 3,000 ukilinganisha na mwaka 2014, waliopata daraja la pili wameongezeka 1,000 na wale wa daraja la tatu wameongezeka 2,000.
 
"Kwa hiyo hakuna athari sana, labda tusipojipanga vizuri baadhi wanaweza kukosa nafasi za kidato cha tano, kwa hiyo ni kama wanafunzi 6,000 kwenye madaraja hayo wameongezeka ulinganisha na mwaka jana, ingawa asilimia imeshuka na hii ni kwa sababu mwaka huu kulikuwa na ongezeko la wanafunzi 150,000 waliofanya mtihani huo,” alisema Prof. Ndalichako.
 
TAMONGSCO
Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco) Kanda ya Dar es Salaam, Moses Kyando, alisema shule ambazo matokeo yake ni ya wastani na zile ambazo zina ada kubwa, zitaathirika kwa kiasi kikubwa.
 
Alisema baadhi ya zile ambazo zimepata matokeo mazuri, zinaweza zisiathirike sana kwa kuwa wanafunzi wengi watarudi kwenye shule hizo kuendelea na masomo ya kidato cha tano.
 
“Lakini si shule binafsi tu, hata za serikali zitaathirika,” alisema.
 
Alisema idadi ya wanafunzi 27,000 ambao mwaka jana hawakuingia kidato cha tano si kwamba walikosa nafasi, bali walipelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma kusomea ualimu ili kuziba pengo la walimu wa Sayansi na Kingereza.
 
“Shule za binafsi nyingi zitakosa wanafunzi kwa sababu waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu si wengi, kwa hiyo wengi watakwenda kwenye vyuo vya diploma na cheti. 
 
"Ninachoweza kusema tu ni kwamba elimu ni janga, na haya mambo ya elimu bure yataongeza watakaofeli kidato cha nne mwaka huu, kwa sababu kile kidogo walichokuwa wanapewa na walimu kwa muda wa ziada hawakipati tena na serikali sasa inaangalia wazazi na wanafunzi na kusahau walimu,” alisema.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa umoja huo Taifa, Benjamin  Nkonya, alisema ni wazi kwamba shule binafsi zitakuwa na wanafunzi wachache kulingana na mahitaji yao.
 
“Lakini sisi tunaangalia hii nchi tunaipeleka wapi. Kipimo cha ubora wa elimu ndiyo tunakitaka sisi. Serikali itatusikiliza tukisema mwanafunzi akipata wastani wa chini ya 40, arudi kuchimba magugu kwao au apelekwe VETA (Chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi).
 
 
Wawekeze zaidi kwenye elimu, shule ambayo haina maabara, walimu, ifutiwe usajili, walimu wapewe mshahara mzuri,” alisema.