Update:

Halmashauri Arusha yatumbuliwa `majipu'

Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo, ameipiga `memo' Kamati ya Wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Arusha akitaka maelezo ya kina kuhusu kuchelewa kukarabati madarasa manne ya Shule ya Msingi Kisimani yaliyoezuliwa na upepo Desemba, mwaja jana.
 
 Akikagua madarasa ya shule hiyo iliyopo kata ya Muriet jijini hapa  jana huku akiwa ameongozana na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la  Arusha, Naibu Waziri Jaffo alisema huo ni  uzembe.
 
“Huu ni uzembe wa hali ya juu ambao hauwezi kuvumilika.
Ingekuwa shule hii ipo halmashauri nyingine zisizo na mapato mengi, sawa, lakini ipo hapa Jiji la Arusha lenye mapato mengi,” alisema.
 
“Nataka maelezo kwa nini leo (jana) hii mafundi wameanza kazi. Pili kwa nini msichukuliwe hatua,” alisema.
 
Alisema maelezo hayo yawe yamemfikia waziri mwenye dhamana leo Jumatatu kwa kila kiongozi wa Kamati ya Wataalam wa Halmashauri (CMT).
 
Tangu kuezuliwa kwa madarasa hayo na upepo Desemba 14, mwaka jana, wanafunzi wamekuwa wakiyatumia madarasa hayo kwa masomo nyakati za mvua na jua.
 
Naibu Waziri Jaffo alianza ziara yake Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kusomewa taarifa ya Halmashauri ya Jiji kuhusu elimu.
 
Katika taarifa hiyo, ilibainika kuwa Idara ya Manunuzi ya
halmshauri hiyo ndiyo iliyochelewesha mchakato wa kumpata mkandarasi wa ukarabati huo.
 
Pamoja na maelezo yaliyotolewa na Ofisa Manunuzi, Seif Kasoli, kuwa hapakuwa na ucheleweshaji wa mchakato wa kumpata mkandarasi, Naibu Jafo aliwaamuri vigogo hao wa halmashauri kumpeleka shuleni hapo ili  akajiridhishe.
 
Hata hivyo, Kasoli alipata wakati mgumu kujieleza kwanini alichelewa kulishughulikia suala hilo kwa dharura.
“Naona tatizo lipo kwa huyu Ofisa Manunuzi,” alisema na kumgeukia Kasoli na kumhoji: “Hivi unatosha kuwa katika nafasi hiyo kweli?”
 
Baada ya kufika shuleni hapo, alishuhudia ukarabati ukiwa ndiyo kwanza umeanza hali iliyomfanya apigwe butwaa.
 
“Hii mbao mmezileta leo baada ya kusikia Jaffo anakuja, kwa nini,” alihoji.
 
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alitembelea Soko Kuu la Arusha, ambapo aliwapongeza kwa kuanza kukusanya mapato kwa mfumo wa kieletroniki.
 
Alitaka mfumo huo utumike pia kwa zahanati ili kukusanya mapato zaidi.

No comments