Update:

Burundi: Ban kukutana na Pierre Nkurunziza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon


Wiki chache baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Burundi inajiandaa kumpokea Jumatatu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye atakua ziarani nchini humo.


Lengo la ziara hii ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni kuisaidia nchi hii iliotoka katika vita viliodumu zaidi ya mwongo mmoja, kutotumbukia tena katika machafuko mapya, wakati ambapo nchi hii inakumbwa na vurugu tangu Rais Pierre Nkurunziza kuchukua uamuzi wa kuwania mhula wa tatu mwezi Aprili 2015.

Lakini ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaonekana kuwa utakua na kazi kubwa nchini humoi. Nchi ya Burundi kwa sasa inakabiliwa na hali ya sintofahamu kutokana na vurugu zinazoendelea, huku serikali ya Bujumbura ikikataa mazungumzo na upinzani ulio uhamishoni nje ya nchi, pia serikali ya Bujumbura imekataa kutumwa nchini mwake kwa kikosi cha askari wa kulinda amani cha Umoja wa Afrika na maandamano yenye uchochezi wa chuki na uhasama dhidi ya Rwanda na rais wake, ambaye anatuhumiwa kulilipatishia mafunzo na kulisaidia kijeshi kundi jipya la waasi wa Burundi.

Ban Ki-moon anatazamiwa kuwasili mjini Bujumbura Jumatatu hii alasiri kwa ziara inayosubiriwa kwa hamu na gamu katika nchi hii ya Maziwa Makuu inayokabiliwa na mgogoro wa kina wa kisiasa kwa karibu miezi kumi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Burundi, Alain-Aimé Nyamitwe, wanasiasa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanasiasa wa upinzani ambao wamebaki nchini.

Pia Ban Ki-moon atakutana Jumanne hii asubuhi na Rais Pierre Nkurunziza. Mazungumzo kati ya wawili hawa yatachukua masaa kadhaa kwa mujibu wa vyanzo vya Umoja wa Mataifa. Ban Ki-moon atajaribu kumshawishi Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ili waeze kukubali mazungumzo yatakayowashirikisha wadau wote bila masharti.

Haki za binadamu

Wasiwasi mwingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atashughulikia suala la "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Burundi". "Tunaamini kwamba atafanikiwa kumshawishi rais wa Burundi kukubali uchunguzi wa kimataifa kuhusu madai hayo," alisema mwanadiplomasia mjini Bujumbura.

Leo, jamii ya kimataifa "inakaribisha ishara ndogo iliyotolewa na utawala wa Burundi kabla ya ziara hii," alisema mwanadiplomasia huyo, akimaanisha hasa kwa kufuta vibali kadhaa vya kimataifa vya kukamatwa dhidi ya wapinzani, kufungua upya vituo viwili vya redio binafsi au pia kukubaliwa kwa ujumbe wa wataalam watatu walioteuliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu. Kwa hiyo kila mtu ana matumaini kwamba Pierre Nkurunziza atakubali.

No comments