Update:

Wanafunzi Mzumbe wapata ufadhili

Mweyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee, Hatim Karimjee (kushoto), akimkabidhi zawadi ya cheti cha ufadhili wa masomo ya Chuo Kikuu, John Method. PICHA: HALIMA KAMBI
 Taasisi ya Karimjee Jivanjee, imewatunuku nafasi ya masomo wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzumbe, Edmund Luguku na John Method, baada ya  kushinda tuzo  ya mwaka 2015 ya wanasayansi chipukizi Tanzania (YST).
 
Wanafunzi hao walishinda tuzo hiyo baada ya kufanya utafiti wa kisayansi juu ya kupunguza matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.
 
Washindi hao walipokea zawadi ya fedha na tiketi ya safari  kwenda kushiriki shindano la wanasayansi chipukizi nchini Ireland kwa gharama ya Ubalozi wa Ireland.
 
Meneja wa Karimjee Jivanjee, Devotha  Rubama, alisema hayo  jijini Dar es Salaam jana, wakati wa maandalizi ya washindi hao kusafiri kwenda  Dublin, Ireland kwa ajili ya shindano hilo.
 
Alisema mashindano ya sayansi na teknolojia hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupenda masomo ya sayansi.
 
“Tunawashukuru YST kutupatia heshima hii. Tunaamini elimu ni kitu muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa, hususan elimu ya sayansi na teknolojia,” alisema.
 
Mwenyekiti wa Karimjee, Hatim Karimjee, alisema mtazamo wa taasisi hiyo ni kusaidia taasisi za elimu kwa kuboresha uwezo   baada ya familia hiyo kuanzisha taasisi nyingi na kutoa misaada kabla ya uhuru.
 
“Tumejenga shule, hospitali, zahanati na vituo vya huduma za jamii, ukiwamo ukumbi wa Karimjee, ambao umetolewa kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,” alisema.
 
Mkurugenzi na mwanzilishi mwenza wa YST, Gozibert Kamugisha, alisema taasisi ya Karimjee huwafadhili Watanzania kusoma katika ngazi ya shahada na shahada ya uzamili nchini.
 
Alisema taasisi hiyo ilianza kufadhili YST tangu mwaka 2012 katika nyaja za teknolojia na utoaji ufadhili wa masomo kwa baadhi ya wanafunzi wanaoshiriki mashindano kila mwaka.
 
“Kwa miaka minne sasa,  Karimjee imetoa udhamini wa masomo ya chuo kikuu kwa wanafunzi 15 ambao walishiriki mashindano ya YST. Hivi sasa wanaendelea na masomo ya udaktari, baioteknolojia na kompyuta,” alisema.