Update:

Sumaye atua Mabwepande kuokoa shamba lake

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
 Hatimaye Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amejitokeza kutetea shamba lake lililovamiwa na wananchi zaidi ya 100 ambao waliojikatia vipande vipande Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
 
Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 33 lilivamiwa na wananchi hao mwishoni mwa mwaka jana na kujigawia na wengine kuuza.
Sumaye jana alijitokeza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambapo alionyesha hati halali za umiliki wa shamba hilo.
 
Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye alikuwa ameambatana na mkewe, alieleza mbele ya kikao hicho kuwa amekuwa akililipia shamba hilo kila mwaka kama sheria inavyotaka.
 
Aidha, Sumaye alisema amekuwa akiliendeleza shamba hilo kwa kulilima hadi pale serikali ilipobadilisha matumizi ya ardhi eneo hilo na kuongeza kuwa yeye ni mmiliki halali wa shamba hilo na alikuwa nalo tangu mwaka 1998.
 
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya awamu ya tatu, 1995-2005.
 
Alisema alifuata taratibu zote mpaka akapata hati na kwamba baada ya serikali kubadili matumizi ndipo naye alipoacha kulilima na kuamua kutafuta matumizi mengine.
 
“DC baada ya utaratibu wa serikali kubadilika, nimeamua pale kijengwe chuo kikuu, nimeona nitafute utaratibu wa kuweka taasisi pale," alisema Sumaye.
 
"Hii inachukua muda. Lazima utafute watu ili uingie nao ubia, hii ndio dhamira yangu ya eneo hili.
 
"Nimeshawaambia hata wale ninaoshirikiana nao kuwa linafaa kwa matumizi hayo.”
 
Kuhusu kauli za wananchi na Diwani wa Mabwepande, Susan Massawe kuwa shamba hilo lilikuwa pori na kusababisha wanawake kubakwa, Sumaye alisema kama ni hivyo alikuwa na haki ya kuarifiwa ili alifyeke na siyo kuruhusu watu wavamie.
Hata hivyo, alikiri kwamba hajalilima shamba hilo kwa miaka mitatu iliyopita.
 
“Kauli eti kuna mtu ana heka 30 lichululiwe, kuna watu wana heka 1,000,000, hao mtafanyaje? Mtakuwa mnavamia mashamba yote? Tukivamia hata nyie mnaovamia mtavamiwa kama tutaruhusu uvamizi, maana watu wenye nguvu nchi hii wapo, hawa wenye silaha wakiamua kuvamia mtawafanyaje?
 
“Jawabu la tatizo si mabavu, tukianza kushindana kwa mabavu watu wataumia sana, kama kulikuwa na tatizo ningeitwa, hebu hapa tunafanyaje lakini siyo kuvamia vamia," alisema Sumaye.
 
"Watu wanaenda mbali wanasema uongo, sasa kama kiongozi anasema uongo hatuwezi kuendeleza nchi kama viongozi.” 
 
Makonda aliwataka wananchi wote waliovamia mashamba ya watu waondoke mara moja, lakini kwenye mgogoro wa shamba la Sumaye aliomba wananchi wampe wiki mbili ili akutane na viongozi waone namna ya kuwasaidia wananchi hao.
 
“Suala la Sumaye kutoliendeleza tutaangalia sheria inasemaje, kama Sumaye amefuata utaratibu wote wa umiliki akipenda anaweza kuwapa sehemu ya shamba hilo lakini hilo atalifanya kwa mapenzi yake,” alisema Makonda.