Update:

Shashamra Mapinduzi Zanzibar zaanza kwa usafi wa mazingira


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto), akizoa takataka wakati akishiriki ufanyaji usafi wa mazingira katika eneo la Soko la Mbogamboga Mombasa, mjini Zanzibar jana.
 Sherehe za kuhadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeanza visiwani hapa kwa viongozi wa kitaifa na wananchi kushiriki kazi za usafi wa mazingira katika maeneo ya huduma za jamii, pamoja na makazi ya watu.
 
Katika wilaya ya Mjini, wananchi wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, mwishoni mwa wiki walisafisha mitaro ya kupitisha maji machafu pamoja na kukusanya taka ngumu kuanzia maeneo ya Uwanja wa Farasi Zanzibar.
 
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Balozi Seif alisema Zanzibar imefanikiwa kuangamiza maradhi ya malaria kwa asilimia 99 na kuwataka wananchi kuungana na kwa hamasa kufanya usafi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi ili kungamiza magonjwa yote yanayosababishwa na uchafu na kuifanya Zanzibar kuwa na mandhari ya kupendeza zaidi.
 
“Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameathiri nchi nyingi duniani ikiwamo Tanzania, ni vyema Zanzibar ikatenga siku maalum ya usafishaji wa mazingira na kuboresha mazingira ili kupunguza athari hizo,” alisema.
Katika kazi hiyo ya usafi wa mazingira, pia Balozi Seif alikabidhi vifaa mbalimbali vya usafi wa mazingira  kwa kikundi cha Usafi wa Mazingira cha Kilimani cha mjini hapa.
 
Vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh. 700,000  vimetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Idara ya Mazingira, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu waliojipangia wa kutoa vifaa kama hivyo kila mwaka kwa vikundi vilivyoonyesha juhudi katika kushiriki  kwenye usafi wa mazingira maeneo mbalimbali.
 
Kiongozi huyo alishiriki usafishaji wa mtaro unaotumika kusafirisha maji machafu kutoka katika maeneo ya Muembe Njugu, Kwahani, Kariakoo, Kilimani na kumalizikia Pwani ya Kilimani.
 
Wapiganaji wa vikosi vya mafunzo, Jeshi la Kujenga Uchumi, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, Zimamoto na Uokozi, Valantia, vikundi vya usafi wa mazingira, watendaji wa baraza la manispaa na wananchi walijitokeza kwa wingi kushiriki shughuli hiyo ya usafi.