Update:

06 January 2016

Nauli za mabasi yaendayo kasi zisiwe mzigo kwa wananchi

 Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra-CCC), limepinga vikali nauli zilizopendekezwa na kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT) kwa ajili ya mabasi yaendayo kasi. Baraza hilo lilipinga nauli hizo juzi wakati wa kikao kilichohusisha wadau wa usafiri na wananchi jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kiliitishwa kwa ajili ya kujadili nauli zilizopendezwa na UDA-RT kwa ajili ya huduma za mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam. Nauli zilizopendekezwa ni kiasi cha Sh.
 
 700 kwa njia za mlisho, Sh. 1,200 kwa njia kuu na Sh. 1,400 kwa mlisho wa njia kuu. Sumatra-CCC imepinga nauli hizo kwa maelezo kuwa ni za juu kutokana na ukweli kuwa watumiaji wengi wa usafiri huo ni walalahoi.
 
Hata hivyo, UDA-RT wanapinga malalamiko hayo wakidai kuwa nauli waliyopendekeza itawasaidia kumudu gharama za uendeshaji wake. Sababu mojawapo wanayoeleza kuwa ni mabasi hayo hayatakuwa yanasubiri abiria vituoni na kulazimika nyakati fulani kubeba abiria wachache kutokana na muda.
 
Pia wanadai kuwa mabasi ni ya kisasa, ambapo ni gharama kubwa kuyaendesha. Hata hivyo, pamoja na yoye, tunadhani kuwa serikali inapaswa kulisimamia suala hili kwa kuangalia hali ya mwananchi mwenye kipato kidogo.
 
Bahati nzuri serikali imeliona hili na kutoa taarifa kupitia Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, kuwa haijaridhia mapendekezo hayo ya nauli kwa kuwa mradi huo ulianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa waishio nje ya jiji.
Moja ya madhumuni makubwa ya serikali kuanzisha huduma za usafiri wa umma ni kusaidia watu wenye kipato kidogo wasiomudu kununua magari. Pia ni mfumo mzuri wa kupunguza msongamano wa magari ikiwa huduma zitatolewa vizuri kwani zitafanya hata wenye magari kuyaacha majumbani.
 
Serikali ilipaswa kuangalia suala la usafiri wa umma kama huduma kwa wananchi wake na sio suala la watu kuachiwa kutengeneza faida kubwa. Suala la utoaji wa huduma za usafiri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam halijaanza leo, kwani wakati wa kipindi cha utawala wa kikoloni wa Mwingereza ilikuwapo Kampuni ya Stage Coach kabla ya kuundwa kwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) baada ya uhuru ili kutoa huduma ya usafiri. Kwa kuwa wananchi wanafanya shughuli mbalimbali zinazoliingizia taifa kodi, basi iangalie kuwa suala la usafiri kama huduma ya kuwasaidia wananchi kufika maeneo ya uzalishaji na si biashara. Madhumuni ya kuanzishwa kwa mradi huu wa mabasi yaendayo kasi ilikuwa kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam. Sio siri suala la foleni katika jiji la Dar es Salaam limekuwa kero kubwa katika maisha ya kila siku katika jiji hili. Hali hiyo inachangiwa zaidi kutokana  na uchache wa barabara uliochangiwa zaidi na mipango miji mibovu.
 
Bahati mbaya idadi ya wakazi za jiji la Dar es Salaam imekuwa ikiongeza, huku kukiwa na mipango miji mibovu.
 
Matokeo yake namba ya wakazi imekuwa kubwa na maana yake idadi ya watu wanaomiliki magari imeongezeka zaidi.
 
Moja ya madhumuni makubwa ya utoaji wa usafiri kwa umma ni kurahisisha watu kutoka upande mmoja kwenda mwingine, hivyo tunashauri serikali isimamie jambo hili kuhakikisha kuwa huduma ya mabasi yaendayo kasi inalenga kusaidia wananchi wa kuanzia wa kipato cha chini hadi juu.
 
Itakuwa jambo la kusikitisha ikiwa nauli kubwa zitatozwa kwenye mabasi hayo na kufanya wananchi kushindwa kumudu. Tunakubaliana na hoja kuwa gharama za uendeshaji wa mabasi hayo ni kubwa, lakini tukumbuke kuwa hii ni huduma kwa wananchi. Serikali inakusanya kodi kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na wananchi hao, ndio maana tunaomba serikali, Sumatra -CCC na UDA-RT wakae na kupanga bei zitakazosaidia wananchi kumudu gharama zake ili lengo la kuboresha usafiri wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam litimie