Update:

Msaidizi wa IGP Mangu, familia yake wafa kwa kusombwa maji

 Watu wanane akiwamo Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Inspekta Gerald Ryoba na familia yake, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo la Kibaigwa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
 
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, David Misime, Ryoba na familia yake wakiwamo mke na watoto wawili pamoja na msichana wa kazi, walikuwa wakitokea mkoani Geita kuelekea jijini Dar es Salaam kwa kutumia gari lenye namba za usajili T516 DEP aina ya Toyota RAV4 iliyokuwa ikiendeshwa na Koplo Ramadhan.
 
Aliwataja marehemu waliokuwapo katika gari hilo kuwa ni msaidizi huyo wa IGP Mangu, watoto wake ambao ni Gabriel Gerald Ryoba, Godwin Gerald Ryoba na mkewe Fidea John Kiondo.
 
Wengine ni dereva wa gari hilo, F 3243 Koplo Ramadhan, msichana wake wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sarah mwenyeji wa Mbinga mkoani Ruvuma.
 
Akifafanua kuhusu tukio hilo, Kamanda Misime alisema lilitokea juzi saa 3:00 usiku eneo la Kibaigwa maarufu kama Bwawani wilayani Kongwa.
 
Aliongeza kuwa baada ya kupewa taarifa kwamba kuna maji mengi eneo hilo na kusababisha magari kushindwa kupita, walifika hapo na kushuhudia hali halisi kisha wakazuia magari yaliyotaka kuendelea na safari.
 
Alisema maji hayo yalikuwa yakitiririka kutoka maeneo ya Njoge na Hembahemba na baada ya kufika eneo la tukio walipata taarifa kuwa kuna gari limesombwa na maji hayo.
 
“Lakini baadaye tulipokea taarifa kuwa kuna gari limesombwa na maji na matairi yapo juu, tulianza kufuatilia na tukazuia magari kupita na baada ya maji kupungua, ndipo tulipoyaruhusu magari kupita,” alisema Kamanda Misime.
 
Aidha, alisema walianza pilikapilika za kulitafuta gari hilo na baadaye usiku wa manane walifanikiwa kulipata.
 
Kamanda Misime alisema baada ya kulitoa kwenye maji, walikuta miili ya watu wawili.
 
“Gari lilikuwa limepondeka pondeka, hivyo tulilazimika kulikata na ndipo tulipofanikiwa kutoa mwili wa Fidea John Kiondo, ambaye ni mke wa Inspekta wa Polisi Gerald Ryoba na pia alikuwa Mwalimu wa Manispaa ya Temeke,” alifafanua Kamanda Misime.
 
Hata hivyo, alisema walipata taarifa kuwa katika gari hilo,  kulikuwa na watu sita, jambo lililowafanya waendelee na harakati za kutafuta miili mingine.
 
“Baadaye tulifanikiwa kupata mwili wa dereva wa gari hilo, F 3243 Koplo Ramadhan ambaye naye alifariki dunia na tukaendelea kutafuta kisha tukapata mwili wa mtoto mwenye umri wa miaka minne Gabriel Gerald Ryoba na hatimaye tukapata mwili wa Godwin Gerald Ryoba,” alisema Kamanda Misime.
 
Alisema mwili wa Ispekta Ryoba ulipatikana jana saa 4:20 asubuhi na pia katika gari hilo kulikuwa na msichana wa kazi aliyefahamika kwa jina la Sarah.
 
“Kwa hiyo miili ya watu wote sita waliokuwa kwenye gari hilo,  tulifanikiwa kuipata, lakini wakati tukiendelea kutafuta kwenye mkondo huo wa maji, tulipata miili mingine miwili, na hivyo kuwa na miili minane,” alifafanua Kamanda Misime.
 
Alisema miili hiyo mingine miwili, mmoja ulitambulika kwa jina la Ludege ambaye ni Ofisa Mifugo kata ya Pandambili Kongwa na mwingine haujafahamika.
 
“Tumeacha taarifa kwa wananchi mbalimbali, inaonekana hayo maji yameanzia mbali na yalikuwa mengi sana, inawezekana kuna watu wengine pia wamesombwa na maji, tumewataka watupe taarifa ili twende kuwachukua,” alisema Kamanda Misime.
 
Alisema kwa sasa jeshi hilo linajiandaa kusafirisha miili ya familia hiyo.
 
“Huyu Koplo ambaye alikuwa ni dereva, ni mwenyeji wa mkoani Lindi na Inspekta ni wa Geita, hivyo tunatarajia kusafirisha mwili wake pamoja na wa mkewe na wa watoto wake wawili na msichana wa kazi atapelekwa kwao Mbinga,” alisema Kamanda Misime.
CHANZO: NIPASHE