Update:

05 January 2016

Magufuli aibua vitanzi 13 ufisadi

 Vigogo 'wapigaji hela' sasa wakosa pa kutokea
Rais John Magufuli
 Katika kile kinachoonekana kuwa ni mwendelezo wa vita dhidi ya vitendo vya kifisadi, Rais John Magufuli ameibua mbinu mpya ya kuwalazimisha watumishi wote wa nafasi za juu kwenye ofisi za umma kusaini kiapo maalum cha uadilifu chenye masharti 13 ambayo yakitekelezwa vyema yataziba mianya yote ya ubadhirifu wa fedha za umma.
 
Katika kiapo hicho cha aina yake na ambacho Nipashe imefanikiwa kuona nakala yake, kila mtumishi wa umma ametakiwa kusoma kwa umakini masharti yote yaliyomo na kisha kusaini kabla ya kuwasilisha kwa mamlaka ya juu yake.
 
Kiapo hicho, ni kile ambacho awali kiliibuliwa Agosti 14, 2015 katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), uliosainiwa na Rais wa Serikali ya awamu ya nne, Jakaya Kikwete, lakini utekelezaji wake umeongezeka na unaonekana kushika kasi zaidi sasa chini ya Rais Magufuli aliyeapa kupambana na ufisadi kwa nguvu zote. 
 
Afisa Habari wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheiba Bulu, alilieleza gazeti hili kuwa nia na dhumuni la kuanzishwa kwa kiapo hicho ni kukuza maadili kwa watumishi wa umma pamoja na kupambana na rushwa kwa watumishi.
 
Wakizungumza na Nipashe kwa sharti la kutoandikwa majina yao, baadhi ya vigogo katika ofisi kadhaa za mashirika na taasisi za umma, wamekiri kupokea nakala za ‘kiapo’ hicho kutokana na maelekezo ya Ofisi ya Rais na kwamba, kufikia Ijumaa ya Januari 15, kila mmoja anatakiwa awe tayari ameshasaini na kufikisha kwa bosi wake.
 
Katika nakala mojawapo ya kiapo hicho cha uadilifu, ambacho baadhi ya wakuu wa taasisi na mashirika ya umma wamekisambaza tangu Desemba 28, mwaka jana, inaonyesha kuwa kila mtumishi anatakiwa awe amesaini na kuzingatia kwa vitendo mambo yote 13 yaliyoainishwa, huku waraka huo (kiapo) ukiwa na anuani isemayo “Ahadi ya uadilifu kwa watumishi wa umma (Kwa utumishi wa umma uliotukuka)”.
 
Aidha, uchunguzi zaidi wa Nipashe umebaini kuwa ‘kiapo’ hicho, kwa kiasi kikubwa kinafanana na kile ambacho makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu walichoapishwa na Rais Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita kwa sharti la kutakiwa wasome wenyewe kila kipengele na kukielewa kabla ya kusaini na kwamba yeyote asiyekuwa tayari kusaini akae pembeni na kuwapisha ili wengine waendelee na kazi. 
 
Hata hivyo, tofauti kubwa iliyopo ni kwamba, ‘kiapo’ cha makatibu na naibu makatibu, kina vipengele 12 wakati cha watumishi kina vipengele 13 na pia, baadhi ya vipengele hivyo vimetofautiana.  
 
“Kiapo hiki ni kipya kwangu. Katika miaka zaidi ya 30 ya utumishi wangu sijawahi kupewa kitu kama hiki na kulazimishwa kusaini. Nadhani ni jitihada za Rais Magufuli kuhakikisha kuwa wote tunachapa kazi zaidi na pia kila mmoja anajiepusha na vitendo vya rushwa,” mmoja wa watumishi wa ngazi za juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliliambia Nipashe mwishoni mwa wiki.
 
“Tulisambaziwa tangu Desemba 28. Tumeambiwa ni lazima tusome kwa umakini kila kipengele na kusaini makubaliano haya kabla ya kuwasilisha ifikapo Januari 15… yale yaliyomo ndani ya makubaliano haya ni mazito. Inavyoelekea wengi tutanyooka kwa sababu inaelezwa wazi kuwa yeyote asiyezingatia masharti anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria,” kigogo mwingine aliliambia Nipashe.
 
VITANZI 13
Mashati ambayo mtumishi wa umma atatakiwa kukiri  ni pamoja na “Nitakuwa Mzalendo kwa nchi yangu na mtii kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Nitahudumia umma na watumishi wenzangu kwa heshima; Nitatimiza wajibu wangu kwa kutoa huduma bora kwa umma; Nitatoa huduma bora kwa usawa kwa watu wote na kutofanya ubaguzi kwa misingi ya dini, siasa, kabila, udugu, ukanda, jinsia, urafiki au hali ya mtu.
 
Mengine ni “Sitatoa, kushawishi, kutoa wala kupokea rushwa; Sitaomba, kutoa wala kupokea zawadi au fadhila za kiuchumi au za kisiasa au kijamii zisizoruhusiwa na Sheria; Sitatumia madaraka yangu kwa manufaa binafsi ya undugu, urafiki au jamaa zangu; nitatekeleza wajibu wangu kwa kufuata sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma; Nitafanya kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu; nitalinda na kutumia rasilimali za umma kwa manufaa ya umma;
 
Masharti mengine ni “Nitaepuka tabia ambayo inavunja heshima ya utumishi wa umma hata ninapokuwa nje ya mahali pa kazi; Sitatoa siri za serikali au za mteja kwa watu wasiohusika isipokuwa kwa maslahi ya umma; Nitajiepusha na mgongano wa maslahi na pale utakapojitokeza nitautatua kwa maslahi ya umma.
 
Aidha, vigogo wamebanwa zaidi pia kupitia kiapo chao chenye masharti 12, baadhi yakiwa ni “Sitatumia cheo changu au wadhifa wangu kwa maslahi binafsi, ya familia yangu, ndugu zangu au marafiki zangu isipokuwa kwa maslahi ya umma; Sitaomba, kushawishi, kutoa wala kupokea rushwa.
 
Vilevile, sehemu ya masharti 14 kwa sekta binafsi yanaeleza kuwa “Hatutashawishi, kuomba, kupokea au kutoa hongo au aina yoyote ile ya Rushwa; Hatutatoa, kuwezesha, kushawishi au kutoa zawadi kwa afisa yoyote wa umma familia zao au washirika wao wa kikazi katika shughuli inayohusiana na mchakato wa manunuzi au katika utekelezaji wa mkataba;
 
TAMKO ZITO
Kadhalika, kila mtumishi wa serikali, atatakiwa kutamka tamko mara baada ya kusoma masharti hayo linalosema “Ninakiri kwamba nimeisoma Hati hii ya Ahadi ya Uadilifu kabla ya kuweka sahihi. Ninakubaliana na kutambua kwamba masharti yaliyopo katika hati hii ni ya kimaadili na kisheria na ninawajibika kuyatekeleza.
 
"Ninaelewa kwamba ukiukwaji wa masharti hayo ni ukiukwaji wa maadili yaliyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, masharti ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sheria ya Utumishi wa Umma, Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sheria ya Kudhibiti Mgongano wa Maslahi na Sheria nyingine za nchi na hatua za kinidhamu na kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yangu iwapo nitakiuka masharti hayo.
 
UFAFANUZI SEKRETARIETI YA MAADILI
Afisa Habari wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheiba Bulu, alisema hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma imegawanyika katika sehemu tatu.
 
Alisema hati ya kwanza inawahusu viongozi wa umma ambao wanahusika na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, na ya pili inawahusu watumishi wa umma, huku ya tatu ikihusu sekta binafsi.
Alisema viongozi wa umma wakishasaini na kuapa wanapeleka fomu zao kwa Kamishna wa Maadili, huku watumishi wa umma wakipeleka kwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara.
 
Aliongeza kuwa, sekta binafsi wanawasilisha fomu zao za ahadi ya uadilifu kwa Mtendaji Mkuu Brela ambaye ndiye Msajili wa Kampuni.
 
Aliongeza kuwa kwa sekta binafsi endapo wataenda kinyume cha masharti hayo, kampuni husika itakuwa imepoteza sifa ya kufanya kazi na serikali.
Alisema fomu hizo za ahadi zilianza kutolewa tangu Oktoba mwaka jana, na watumishi wa umma walitakiwa kuzirudisha Desemba 31, mwaka jana wakiwa na fomu za tamlo la rasilimali na madaraka yao.
 
AHADI YA MAGUFULI VITA DHIDI YA UFISADI
Wakati wa kampeni za kuwania kiti cha urais, Dk.  Magufuli aliwahi kusema “Nitasimamia uundwaji wa Mahakama ya kushughulikia Mafisadi na Majizi wa nchi ili wafungwe.”
 
Hivyo, kuanzishwa kwa utaratibu huo wa kuapa kwa ahadi ya uadilifu ni mojawapo ya utekelezaji wake wa kupambana na masuala ya ubadhirifu wa fedha kwa mafisadi serikalini.
 
CHANZO: NIPASHE