Update:

12 January 2016

Kamati za Bunge zaanza kutangazwa.


Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Mchakato wa uteuzi wa Kamati za Bunge, umeenza rasmi baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuteua wajumbe 15 wa Kamati ya Kanuni za Bunge.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, Spika ametumia kanuni ya 116 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013 kuteua kamati hizo.
 
Walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni Makame Kassim Makame, Mbunge wa Jimbo la Mwera;  Tundu Mughwai Lissu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki; Jasson Samson Rweikiza, Mbunge Jimbo la Bukoba Vijijini na Ally Saleh Ally, Mbunge Jimbo la Malindi.
 
Wengine ni Magdalena Sakaya, Mbunge Jimbo la Kaliua; Salome Makamba, Mbunge wa  Viti Maalum; Dk. Jasmine Bunga, Mbunge wa Viti Maalum na Zainab Katimba, Mbunge wa Viti Maalum.
 
Wengine ni Balozi Adadi Rajab, Mbunge, Jimbo la Muheza; Dk. Charles Tizeba, Mbunge Jimbo la Buchosa na Kangi  Lugola, Mbunge Jimbo la Mwibara.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati hiyo imeundwa na kutangazwa kabla ya kamati nyingine ili ifanye marekebisho ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge kuhusu majukumu ya kamati nyingine kwa kuyashabihisha na majukumu ya serikali kwa kuzingatia muundo wa Baraza la Mawaziri lililoundwa na Rais John Magufuli.
 
Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Mwenyekiti wake ni Spika mwenyewe,  Naibu Spika ni Makamu Mwenyekiti na wengine ni Kiongozi wa Upinzani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao ni wajumbe kwa nyadhifa zao na itakutana katika Ofisi ya Bunge, Dar es Salaam Januari 15, mwaka huu,  saa 5: 00asubuhi.
 
Aidha, Spika atakamilisha uteuzi wa wajumbe katika kamati nyingine za Bunge kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa Bunge utakaoanza Januari 26,  mwaka huu, mjini Dodoma ili kutoa fursa kwa kamati zote kuchagua viongozi wake na kuandaa mpango kazi wa mwaka 2016/17.