Update:

JUMAZA yapinga uchaguzi Zanzibar kurudiwa

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA), Sheikh Muhiddin Zuber Muhiddin
 Wakati Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inasubiriwa kutangaza tarehe ya marudio, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) imepinga kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo.
 
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Sheikh Muhiddin Zuber Muhiddin, alipozungunza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ),  Kikwajuni mjini hapa.
Sheikh Muhiddin alisema kutokana na mazingira ya hali ya kisiasa, si wakati muafaka uchaguzi wa Zanzibar kurudiwa na kufanya hivyo kunaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi.
 
“Mtazamo wetu kutokana na hali ya kisiasa ya Zanzibar si busara kurudia uchaguzi. Badala yake viongozi wakae na kuja na ufumbuzi kama serikali ya mpito muhimu kumaliza mkwamo wa uchaguzi kwa amani,” alisema.
Alisema uzoefu unaonyesha kuwa uchaguzi wa marudio mara nyingi huwa haufanyiki katika mazingira ya amani na utulivu na badala yake kutumika nguvu kubwa na vyombo vya dola kusababisha madhara na hali ya wasiwasi kwa wananchi.
 
Aidha, alisema katika Afrika Nigeria, Zimbabwe na Malawi, ziliwahi kurejea uchaguzi lakini zilijikuta zikitumbukia katika machafuko wakati Zanzibar haina historia nzuri ya kisiasa baada ya Mapinduzi na kabla ya kufanyika Mapinduzi mwaka 1964.
 
“Wengi tunakumbuka katika historia ya Zanzibar kile kinachoitwa vita au mchafuko ya Juni, Uchaguzi wa Januari mwaka 1961, ambapo ulisababisha machafuko makubwa ikiwemo vifo vya watu 68, maelfu kujeruhiwa na nyumba kuchomwa moto,” alisema Sheikh Zuber.
 
Alisema baada ya wananchi kusikia Viongozi wa kitaifa na marais wastaafu wamefungua mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mkwamo wa uchaguzi walipata matumaini ya kupatikana ufumbuzi wake kwa wakati.
 
Hata hivyo, alisema bahati mbaya hadi sasa vikao nane vimefanyika tangu kuanza mazungumzo hayo Novemba, mwaka jana, na hakuonekani matumaini yale yaliyokuwa wamejengwa na wananchi.
 
Alisema kuwa ni jambo la kusikitisha mazungumzo hayo kufanyika kwa siri kubwa bila kuzingatia kuwa mgogoro huo unahusu maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.
 
“Vikao hivi vimechukua muda mrefu sana hivyo kuibua maswali mengi na shaka kwa wananchi pamoja na kuibuka baadhi ya wajumbe wanaoshiriki mazungumzo kutoa kauli zinazoshabikia msimamo wa upande mmoja,” alisema.
 
Alisema wakati umefika kwa viongozi wakuu wa kisiasa wanaoshiriki mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi, watoke hadharani na taarifa kwa umma juu hatua iliyofikiwa pamoja na muda wa kukamilika kwa mazingumzo hayo.
 
Alisema inasikitisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wakati waangalizi wa ndani na nje walisema ulikuwa huru na wa haki katika ripoti zao.
 
Pia alisema inashangaza uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 pamoja na kuwa na kasoro nyingi matokeo hayakufutwa pamoja na kupingwa na waangalizi wa ndani na nje.
 CHANZO: NIPASHE