Update:

Ahadi ya kuboresha Reli ya Kati itekelezwe

 Toleo la jana la gazeti hili lilikuwa na habari juu ya kukwama kwa zaidi ya abiria 1,000 wa treni waliokuwa wanatokea mikoa ya Tabora, Kigoma na Mwanza wakielekea Dar es Salaam na Dodoma.
 
Hali hiyo ilitokea kufuatia sehemu ya reli kati ya eneo la Kidete na Msaganza, mkoani Morogoro kuzolewa na maji kufuatia mvua kubwa zinazonyesha katika maeneo hayo na ya jirani.
 
Hali hiyo ilisababisha Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kulazimika kukodi mabasi 17 kwa ajili ya kusafirisha abiria hao kwenda Dar es Salaam.
Abiria hao walikwama kwenye stesheni ya Dodoma baada ya kuwapo kwa taarifa za kuharibika kwa sehemu hiyo ya reli.
 
Hata hivyo, tunapongeza hatua ya uongozi wa TRL ya kutoa fedha ya kujikimu kwa abiria hao na pia kuwatafutia usafiri mbadala.
 
Kufuatia hali hiyo, uongozi wa TRL umetangaza kusitisha usafiri wa treni wa Reli ya Kati kwa kipindi kisichojulikana.
 
Taarifa zilizopo ni kuwa, sehemu iliyoathirika na mafuriko hayo ni kubwa ingawa serikali imeagiza matengenezo yafanywe haraka.
Kitendo hicho cha uongozi wa TRL kusimamisha safari zake ni pigo kubwa kwa watumiaji wa usafiri huo.
 
Hata hivyo, jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa tatizo la eneo la Mzaganza ni la muda mrefu na limekuwa likijirudia mara kwa mara bila ya ufumbuzi wa kudumu kutafutwa.
 
Serikali imefikia wakati lazima ichukue hatua madhubuti za kuhakikisha ufumbuzi wa kudumu unatafutwa.
 
Ni jambo la kusikitisha suala la Reli ya Kati limekuwa likipigiwa debe na wanasiasa kila wanapoomba kura, lakini hakuna uwekezaji wa maana uliowekwa kwenye reli hiyo.
 
Tuna imani, Rais John Magufuli, atatimiza ahadi yake ya kuifanya reli hii kuwa ya kisasa.
 
Kutokana na ukweli kuwa, kama kweli nchi yetu inataka kupiga hatua kimaendeleo lazima zifanyike jitihada za dhati za kuwekeza kwenye usafiri wa reli.
 
Kuna faida nyingi za kiuchumi, mathalani  ni usafiri wa uhakika kama miundombinu yake itawekwa vizuri.
 
Kutokana na uwekezaji mzuri wa miaka mingi, nchi kama Uingereza hupata faida ya kiasi cha pauni za Uingereza bilioni 13 (Sh. trilioni 41 za Tanzania) kwa mwaka kutokana na usafiri huo.
 
Sote tunafahamu kuwa Reli ya Kati ilijengwa na wakoloni wa Kijerumani, lakini jambo la kusitikisha hakuna uwekezaji wa maana kwenye reli hiyo uliokwishafanyika tangu wakati huo.
 
Pamoja na nchi yetu kupata uhuru miaka 54 iliyopita, lakini kumekuwa hakuna uendelezaji wa reli hiyo pamoja na kuwa na watumiaji wengi.
Tunaipongeza serikali kwa kuboresha miundo mbinu ya barabara nchi nzima, lakini tunadhani usafiri wa reli ukiendelezwa utasaidia watu wengi zaidi.
Pia itasaidia kudumu kwa barabara ambazo zimeigharimu serikali fedha nyingi kuzijenga.
Serikali pia kama itaamua kujenga reli ya kisasa, ina maana watu wengi watakuwa wanatumia muda mfupi kufika katika sehemu mbalimbali.
 
Ni hivi karibuni tu, Ethiopia ilizindua treni ya mwendo kasi, kwa hiyo ni suala ambalo linawezekana ikiwa serikali itawekeza vya kutosha kwenye sekta hiyo.
 
Uboreshaji wa Reli ya Kati utasaidia kuondokana na tatizo la kila mwaka la kung’olewa reli kwenye maeneo kama hayo ya Mzaganza.