Update:

Watoto 79 wazaliwa mkesha wa krismas Dar


 Jumla  ya watoto 79  wamezaliwa katika mkesha wa sikukuu ya Krismasi  katika hospitali mbalimbali za jijini Dar es Salaam.
 
Watoto hao waliozaliwa katika hospitali mbalimbalii 45 ni wa kike na 34  wa kiume wakati 25 walizaliwa kwa njia ya upasuaji.
 
Akizungumza na waandishi wa habari Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwanne Yusuph, alisema watoto 13 walizaliwa katika hospitali hiyo tisa wakiwa wakiume na saba wa kike.
 
Alisema watoto kumi  kati ya hao walizaliwa kwa njia ya  upasuaji na watoto wawili kati yao ni njiti.
 
Katika hospitali ya Amana, Afisa muuguzi wa zamu, Florensia Ndumbaro, alisema walizaliwa watoto 33  na kati ya hao wakike ni 15 na wakiume ni 18 na kwamba waliofanyiwa upasuaji ni wazazi nane na watoto wote wanaendelea salama.
 
Naye Afisa Muuguzi Kiongozi wa Hospitali ya Temeke , Rashid Nyombage alisema walizaliwa watoto 12 kati ya hao watoto nane ni wakike na wanne ni wa kiume huku  wawili wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.
 
Alisema hali za watoto hao zinaaendelea vizuri na huduma zimeboreshwa kwa kuwa changamoto zilizokuwepo awali serikali imetatua ikiwemo suala la vitanda.
 
Katika hospitali ya Mwananyamala, Muuguzi wa zamu, Halima Mbano alisema walizaliwa watoto 21 kati ya hao wakike ni 15 na wakiume ni sita huku watano wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.