Update:

Ushindi mkubwa kwa niaba ya paka Uturuki


Mavis
Mavis anaonekana kutokuwa na wasiwasi licha ya masumbuko ya mmiliki wake
Mwanamke nchini Uturuki ameshinda kesi dhidi ya watu waliotaka kumfukuza paka wake kutoka kwa nyumba ambayo yeye amekuwa akiishi kama mpangaji.
Wasimamizi wa nyumba alimokuwa akiishi Aysegul Yetis na paka wake kwa jina Mavis walikuwa wamewasilisha kesi dhidi yake wakisema mizoga na vyakula vingine alivyokuwa akila paka wake vilikuwa vikiudhi wapangaji wengine.
Mahakama ya chini ilikuwa awali imeagiza Yetis aondoe mizoga aliyokuwa akila paka huyo na pia paka huyo aondoke kwenye nyumba hiyo.
Lakini mahakama ya juu imesema watu wanafaa kuwajali wanyama wanaoishi maeneo yao, gazeti la Daily Sabah limeripoti.
"Ni ukatili kwa watu kusumbuliwa na vyakula vya wanyama wadogo kama vile paka,” alisema jaji Gokhan Turhan.
“Upendo na huruma ni haki kuu ambazo zinafaa kujivuniwa na viumbe wote.”
Vyombo vya habari Uturuki vinasema uamuzi huo wa mahakama ni ushindi mkubwa kwa paka na wamiliki wao.
Aidha, utakuwa ukirejelewa katika kesi zinazohusu kutimuliwa kwa wanyama wapenzi.
Licha ya furaha ya kushinda, Bi Yetis anasema kesi hiyo imemwathiri sana kiakili na kifedha.
“Hivi havikuwa vita vya paka wangu pekee. Nilitaka kuhakikisha paka wengine hawatakumbwa na masaibu kama haya.”