Update:

TFDA yatoa angalizo kwa wanunuzi maziwa ya watoto

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Hiiti SIllo, akimuonyesha Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Polisi, Naibu Kamishna Hezron Gyimbi

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Idara ya Upelelezi (DCP), imekamata bidhaa aina ya vyakula vyenye thamani ya Sh. milioni 26.2 ndani ya saa 48 yakiwamo maziwa ya watoto ambayo hayajasajiliwa.

Akizungumzia operesheni hiyo jana, Mkurugenzi wa (TFDA), Hiiti Sillo, alizitaja bidhaa nyingine zilizokamatwa na ambazo hazijasajiliwa na mamlaka husika ni maziwa ya watoto wachanga aina ya SMA, Promil, Gold, Infacare na Isomyl, ambayo yako kwenye kg 126.

Akitolea ufafanuzi katika hilo, alisema vyakula vya watoto vya kusindika vilivyosajiliwa vinapaswa kusomeka katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwenye vifungio kwa mujibu wa kanuni ya mwaka 2013.

Katika ufafanuzi uliotolewa, ilielezwa uingiaji na utokaji wa bidhaa hizo umechangiwa na wasimamizi wazembe walioko mipakani kula nyama na wafanyabiashara wanaoingia na kutoka nchini.

Aidha, bidhaa hizo zimekamatwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, kupitia operesheni inayojulikana kama ‘Fagia1’ iliyoandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pamoja na Tume ya Ushindani (FCC).

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu mipaka, Naibu Kamishna wa Polisi Idara ya Upelelezi, Hezron Gyimbi, alisema ongezeko la bidhaa hizo limechangiwa na wafanyakazi wa mipakani kurubuniwa na kundi linaloingiza bidhaa bandia kutokana na kushindwa kudhibitiwa.

Alisema operesheni hiyo imeyahusu maeneo 124 kati yake ni maduka ya vyakula 29, nyumba za starehe mbili, Supermarket 20, Mini supermarkets 27, maduka ya pombe za vinywaji vikali, ghala moja na maduka 39 ya bidhaa mbalimbali.