Update:

Panga la Magufuli lafyeka kigogo Reli

Rais, Dk. John Magufuli
 Kasi ya Rais, Dk. John Magufuli, katika kufichua ubadhirifu wa fedha katika taasisi za serikali imeshika kasi ,baada ya jana kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito.
 
Kusimamishwa kwa mkurugenzi huyo kumeelezwa ni kupisha uchunguzi  wa kina kutokana na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
 
Kadhalika, Rais Magufuli amevunja Bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL), kutokana na kutoridhishwa na jinsi ilivyoshughulikia ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.
 
Reli ya kati imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu kushindwa kutoa huduma za uhakika kwa wananchi kunakosababishwa na kuharibika mara kwa mara kwa miundombinu.
 
Kutokana na hali hiyo, Rais Dk. Magufuli katika kampeni zake aliwahi kueleza kuwa atajenga reli hiyo kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge).
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alieleza kuwa Rais Dk. Magufuli amefikia uamuzi wa kumsimamisha mkurugenzi huyo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani ‘Standard Gauge’.
 
Balozi Sefue alisema  mbali na Rais Dk. Magufuli kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo, pia ameivunja Bodi ya RAHCO baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika.
 
Rais Magufuli pia amemtaka mkurugenzi  huyo kutoa ushirikiano kwa vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa zabuni hiyo.
Katika kutekeleza agizo hilo, Rais Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo itathibitika kuwa zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria
 
Kusimamishwa kwa Mkurugenzi wa RAHCO kunaongeza idadi ya wakurugenzi watatu wa idara nyeti za serikali waliosimaishwa na Rais Dk. Magufuli katika kipindi cha siku 47 tangu alipoapishwa Novemba 5, ili  kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.
 
Desemba 7, mwaka huu Rais Magufuli alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe, pamoja na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Prof. Joseph Msambichaka na kuivunja Bodi ya Bandari.
 
Desemba 17, mwaka huu pia Rais Dk. Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah.
 
Kadhalika Novemba 27, mwaka huu Rais Dk. Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade.