Update:

Ngoma, Kiiza wamjaza upepo MaguliKINARA wa mabao Ligi Kuu Bara, Elias Maguli anayecheza Stand United, amesema uwepo wa mastraika wakali wa kigeni wanaomfukuzia nyuma yake katika upachikaji mabao kama Donald Ngoma na Amissi Tambwe wa Yanga unamfanya apambane ili aendelee kutesa.

Hata hivyo, Maguli alisema hachuani na nyota hao wa kigeni na badala yake anapambana ili kuisaidia zaidi timu yake iweze kufanya vizuri na kumaliza katika nafasi tano za juu.

Maguli anaongoza upachikaji wa mabao katika ligi akiwa na bao tisa akifuatiwa kwa karibu na Donald Ngoma wa Yanga na Hamis Kiiza wa Simba wenye mabao manane kila mmoja, huku Kipre Tchetche wa Azam na Tambwe wakiwa nyuma yao.

Maguli alisema hafahamu mastraika hao wa kigeni wamejipanga vipi katika kuendelea kupachika mabao, lakini kwa upande wake anatamani aendelee kuifungia timu yake mabao mengi zaidi ili iweze kumaliza katika nafasi hizo za juu.

“Wananipa changamoto ya kuendelea kufanya vizuri, siwezi kuwazungumzia sana kwa kuwa sifahamu wamejipanga vipi,” alisema.