Update:

Mamlaka za kusimamia nyama zidhibiti matumizi ya kemikali


KATIKA toleo la gazeti la jana la Nipashe kulikuwa na habari kuhusu jinsi walaji nyama ya ng’ombe katika Jiji la Dar es Salaam walivyo katika hatari ya kupata maradhi mbalimbali.

Magonjwa yaliyotajwa ni saratani na kushindwa kufanya kazi kwa ini na figo. Hali hiyo inatokana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia kemikali zisizofaa kuwanenepesha wanyama hao kabla hawajafika sokoni.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa miezi kadhaa unaonyesha wafanyabiashara huwalisha mifugo kemikali mbalimbali ikiwamo mbolea ya `urea.’

Nyama ya ng’ombe ni kitoweo kinachotumiwa zaidi katika Jiji la Dar es Salaam.

Inakadiriwa kuwa katika Jiji la Dar es Salaam, wakazi hula tani 120 za nyama sawa na ng’ombe 1,200 kwa siku.

Pia Tanzania husafirisha kiasi cha ng’ombe 300,000 kwenda Kenya baada ya kuchinjwa. Kutokana na kupendwa kwa kitoweo hicho, kumefanya hata mahitaji yake kuwa makubwa zaidi. Hata hivyo, kuna jambo la kusikitisha kuwa kuna ishara za kuwapo kwa upungufu na usimamizi wa biashara ya nyama ya ng’ombe. Hii inatokana na kauli tofauti ambazo zimetolewa na watendaji wa serikali wenye dhamana ya kufanya ukaguzi na kusimamia biashara hiyo ili kuhakikisha nyama inakuwa salama kwa walaji.

Mfano, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi katika Manispaa ya Ilala ambako ndiko kuna machinjio ya Vingunguti na Ukonga, Dk. Audifas Sarimbo, alikaririwa na gazeti hili akisema hakuwa na taarifa juu ya suala la ng’ombe kulishwa kemikali za kunenepesha.

Pia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), nayo ilisema inafahamu kuna dawa maalum za kunenepesha mifugo, lakini walikuwa hawafahamu suala la matumizi ya mbolea kulisha ng’ombe. Tunashauri kuwa mamlaka zinazohusika na kusimamia biashara ya nyama ya ng’ombe, kuhakikisha hatua zinachukuliwa ili kuadhibu wote wanaotumia njia haramu kunenepesha mifugo hiyo.

Vyombo hivi vinapaswa kuwa makini na usimamizi wa biashara ya nyama kwani linagusa afya ya Watanzania.

Tatizo la kunenepesha ng’ombe linatokana na baadhi ya wafugaji kuingiwa na tamaa ya kutaka kutengeneza faida kubwa kwa haraka. Katika biashara ya nyama ya ng’ombe, idara ya mifugo inatakiwa kutimiza jukumu lake kikamilifu kwani ina dhamana ya kulinda afya ya Watanzania.

Idara hii inatakiwa kuhakikisha kuwa nyama inayouzwa inakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani na kisukari na maradhi haya yamekuwa yakichangiwa zaidi na aina ya vyakula.
Kitendo cha kuwapo walakini katika biashara ya nyama ina maana serikali inapaswa kuhakikisha inasimamia mamlaka zake ili zitekeleze majukumu yake inavyotakiwa.

Kwa hili, serikali inatakiwa kuanza na maofisa mifugo ambao wako sehemu mbalimbali nchini kuona wanatimiza majukumu yao kikamilifu.

Mathalan, mfanyabiashara mmoja amenukuliwa na gazeti hili akikiri kuwa anatumia kemikali kunenepesha ng’ombe wake akidai kuwa njia za kawaida za kulisha majani na pumba huchukua muda mrefu kunenepesha ng’ombe.
Ni jambo linalodhihirisha kuwa mamlaka zenye dhamana ya kusimamia biashara hii hazifanyi kazi ipasavyo.

Ni muhimu basi kwa maofisa wa mifugo na TFDA kutimiza majukumu yao kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa usalama.