Update:

Majaliwa: Marufuku mahindi ya msaada kupika pombe


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amepiga marufuku chakula cha msaada kutumiwa kutengeneza pombe za kienyeji na atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika jana katika vijiji vya Nangurugai, Machang’anja na Narungombe katika kata za Mbwemkuru na Narungombe wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja za Diwani wa Narungombe, Rashid Nakumbya, aliyetoa ombi la kuongezewa chakula cha msaada kwa sababu wana hali mbaya.
Alisema msimu uliopita haukuwa mzuri kiuzalishaji kutokana na hali mbaya ya hewa.

Pia aliomba wasaidiwe kuboreshewa huduma za maji safi na salama.
“Natambua kuwa kuna tani 2,000 za chakula zimeletwa katika mkoa wetu, lakini hizo hazitoshi kwa sababu mahitaji yetu ni zaidi ya tani 5,000. Chakula hiki hakitoshi kwa sasa, lakini kitasaidia kupunguza makali ya njaa,” aliwaeleza wakazi hao.

“Tumepiga marufuku kutumia chakula cha msaada kupikia pombe. Mwananchi atakayekutwa akitumia chakula hicho, atachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisisitiza.

Aidha, alirudia kauli ya Rais Dk. John Magufuli, kwamba hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa.

Aliwataka wakazi hao waendelee kuwaombea yeye pamoja na Rais Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, ili watimize malengo waliyoahidi kwa Watanzania wakati wa kampeni.