Update:

Jammeh atangaza Gambia kuwa nchi ya KiislamuGambia

Jammeh aliondoa Gambia kutoka Jumuiya ya Madola 2013

Rais wa Gambia Yahya Jammeh ametangaza taifa hilo lenye Waislamu wengi kuwa jamhuri ya Kiislamu, hatua ambayo anasema inakatiza kabisa uhusiano na historia ya zamani ya kikoloni.

Bw Jammeh ameambia runinga ya taifa kwamba tangazo lake linaambatana na sifa na maadili ya kidini ya Gambia.

Ameongeza kuwa raia na wageni wa dini nyingine hawatalazimishwa kuvalia mavazi ya Kiislamu, na wataruhusiwa kuendelea na dini zao bila kusumbuliwa.

Asilimia 90 ya raia wa Gambia ni Waislamu.

Koloni hiyo ya zamani ya Uingereza hutegemea sana utalii. Uhusiano kati ya taifa hilo na nchi za Magharibi umekuwa ukidorora siku za karibuni.

Muungano wa Ulaya ulikatiza kwa muda pesa za msaada kwa Gambia mwaka jana kutokana na rekodi mbaya ya haki za kibinadamu.

Bw Jammeh ameongoza taifa hilo ndogo la Afrika Magharibi kwa miaka 21.

Mataifa mengine yanayojitambulisha kama jamhuri za Kiislamu ni Iran na Pakistan, na barani Afrika kuna Mauritania.

Bw Jammeh aliondoa Gambia kutoka kwa Jumuiya ya Madola 2013 akitaja muungano humo kuwa wa ukoloni mamboleo.

Mwaka 2007, alidai kuwa alikuwa amepata dawa ya kiasili ambayo ingetibu Ukimwi.