Update:

Jaji Bomani aja na mwarobani wa mgogoro wa ZanzibarAliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu na Jaji mstaafu, Mark Bomani

Aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu na Jaji mstaafu, Mark Bomani (pichani), ameshauri liundwe jopo la wataalam wa masuala ya uchaguzi kubaini na kuzifanyia kazi dosari zilitokea mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

Jaji Bomani amesema jopo hilo lijumuishe wajumbe kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Idara ya Uchaguzi ya Umoja wa Madola, Umoja wa Afrika (AU) na liongozwe na Jaji Mkuu.

Aidha, amesema baada ya kuundwa kwa jopo hilo, daftari la wapiga kura lipitiwe kwa umakini kubaini dosari hizo kisha uchaguzi urudiwe haraka hata ikiwezekana ndani ya siku 30 tangu kuundwa kwa jopo hilo.

Alisema kama mgogoro wa Zanzibar hautapatiwa ufumbuzi haraka, madhara yake ni makubwa kwa taifa kwa kuwa hakutakuwa na serikali halali iliyochaguliwa na wananchi.

Jaji Bomani ametoa kauli hizo ikiwa zimepita siku 73 tangu matokeo ya uchaguzi mkuu kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kwa kile kilichoelezwa kuwapo kwa kasoro kadhaa zilizojitokeza wakati wa kuhesabu na kupiga kura.

Kufuatika kufutwa kwa matokeo hayo, hadi sasa muafaka wa kutatua mgogoro huo visiwani Zanzibar haujapatikana, huku mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, akidai kuwa yeye ndiye mshindi wa uchaguzi huo kwa kuwa alipata kura 200,007 sawa na asilimia 52.87 baada ya chama chake kukusanya fomu za matokeo vituoni na kufanya majumuisho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Jaji Bomani alisema baada kurudiwa kwa uchaguzi huo, jopo hilo litatakiwa liendelee kuwapo wakati wa kurudia uchaguzi ili lishuhudie mwenendo wote wa uchaguzi.

Alisema kabla ya uchaguzi huo kurudiwa, wagombea wote pamoja na vyama vyao wale kiapo kwa kuahidi kukubali matokeo ya uchaguzi uliorudiwa.
Jaji Bomani alisema mgogoro uliopo sasa Zanzibar, hauwezi kupatiwa ufumbuzi bila kufuata sheria na katiba.

“Njia pekee ambayo inaweza maliza mgogoro huu wa Zanzibar ni kwa uchaguzi kurudiwa bila ya kuchelewa, lakini chini ya masharti ya haki, uwazi na yanayoridhisha,” alisema.

Aliongeza kuwa Maalim Seif asiendelee kujitangaza kuwa mshindi na wala asiogope uchaguzi kurudiwa kwani wananchi waliompigia kura hapo awali watarudia kufanya hivyo katika uchaguzi wa marudio na pengine kuongezeka.
Alisema kujitangaza kuwa mshindi, haileti maana yoyote kwa kuwa Zec ndiyo inayomtangaza mshindi kisha kuapishwa na Jaji Mkuu.

AKERWA NA RUSHWA
Jaji Bomani alisema anasikitishwa na vitendo vya rushwa au matumizi ya fedha chafu vilivyokuwa vinatokea wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Alisema baadhi ya wagombea kwa kiasi kikubwa walikuwa wanatumia fedha chafu kama hongo na kushinda uchaguzi, na kueleza hilo jambo linastahili kukemewa na kulaaniwa.

KATIBA MPYA
Jaji Bobani alisema mchakato wa kupata Katiba mpya uendelee, lakini mpaka mgogoro wa Zanzibar utakapotatuliwa na kupatikana kwa serikali mpya.
Kuhusu migogoro ya ardhi na ile ya wafugaji na wakulima, Jaji Bomani alisema serikali inapaswa kuweka kipaumbele cha hali ya juu kwa sekta ya ufugaji kutambuliwa.


CHANZO: NIPASHE