Update:

AU kutuma walinda amani BurundiImage copyright AP Image caption Umoja wa Mataifa unasema watu takriban 400 wameuawa Burundi tangu Aprili

Muungano wa Afrika umetangaza mpango wa kutuma walinda amani nchini Burundi kuzuia machafuko zaidi nchini humo.

Uamuzi huo ulifikiwa baadaye Alhamisi baada ya mkutano mjini Addis Ababa.

Muungano huo umepanga kutuma walinda Amani 5,000 wa kulinda raia.

Umoja wa Mataifa unakadiria watu 400 wameuawa tangu machafuko kuzuka mwezi Aprili Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kwamba angewania urais kwa muhula wa tatu.

AU huenda ikalazimika kutuma walinda amani bila kupewa idhini na taifa mwenyeji, muungano huo utatumia kwa mara ya kwanza kifungu kwenye mkataba wake, kinachouruhusu kuingilia kati katika mataifa mengine nyakati za hatari kubwa.

Baadhi ya mambo ambayo muungano huo unaruhusiwa kuingilia kati kuzuia ni uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu.

Maafisa wa UN wameonya kuwa nchi hiyo inakabiliwa na hatari ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mauaji mabaya zaidi yalitokea Ijumaa wiki iliyopita wapiganaji waliposhambulia maeneo ya jeshi Bujumbura.

Jeshi lilisema watu 87 waliuawa.

AU hata hivyo bado itahitaji kupewa idhini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati.