Update:

Mamia ya Wakenya ‘wajiondoa’ al-Shabab


Al-Shabab

Image copyright n Image caption Wapiganaji wa al-Shabab wamekuwa wakishambulia Kenya mara kwa mara

Watu 700 waliokuwa wamejiunga na makundi ya wapiganaji Somalia wametoroka na kurejea Kenya, ripoti ya Shirika la Kimataifa kuhusu Uhamiaji (IOM) inasema.

Ripoti hiyo inaonya kuwa ni hatari kukosa kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida katika jamii.

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab katika taifa jirani la Somalia limekuwa likisajili watu kutoka eneo la kaskazini mashariki la Kenya.

Kenya imeshuhudia msururu wa mashambulio kutoka kwa wapiganaji hao.

Mapema mwaka huu watu 148 waliuawa baada la wapiganaji wa kundi hilo kushambulia chuo kikuu cha Garissa.

Ingawa ripoti hiyo haijataja watu hao waliorejea Kenya walitoka kwenye makundi yapi, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (Supkem) Hassan Ole Nadu amethibitisha kwamba walikuwa wamejiunga na al-Shabab.

Ripoti hiyo ya kurasa 36 ilitayarishwa na IOM, Supkem na wizara ya masuala ya ndani nchini Kenya.

Watafiti waliohusika kuandika ripoti hiyo waligundua kuwa wengi wa watu wazima waliojiunga na wapiganaji hao walifanya hivyo kwa hiari.

Thuluthi ya watoto waliokuwa wamejiunga na makundi hayo walishurutishwa.

Kurejea kwa vijana hao kunatoa “fursa na pia hatari kwa Wakenya.”

“Kwa upande mmoja wanaweza kutumiwa kukabiliana na mafunzo ya kueneza itikadi kali na pia juhudi za makundi hayo kupata wafuasi, ripoti hiyo inasema.

"Kwa upande mwingine, hatua wanazochukua maafisa wa usalama zinaonekana kuwafanya watu kuzidi kuwa na misimamo mikali kwani wanaorejea wanajihisi kuwa hatarini. Hawana njia bora ya kurudi tena katika jamii.”

Walioshiriki katika utafiti huo walitaja usalama kama jambo linalowazuia zaidi katika juhudi zao za kurejelea maisha ya kawaida katika jamii.

Jumla ya watu 185 walihojiwa, ambao ni karibu 30% ya watu 684 waliorejea Kenya baada ya kuondoka makundi hayo ya wapiganaji.

Wengi walikuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 34.