Update:

Lowassa: Nimejiandaa kuwaongoza WatanzaniaMgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa
Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Rwandanzovwe, Nzovwe mjini Mbeya jana. Picha na Emmanuel Herman 

Mbeya/Mbarali. Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa amesema amejiandaa na yupo tayari kuwaongoza Watanzania akiwa rais wa awamu ya tano.

Akizungumza kwenye Uwanja wa Ruanda Nzovwe- Mbeya Mjini, Lowassa alisema: “Ninatosha, nitumeni kwa kura zenu… nipeni kura za kutosha niwatumikie.”
Lowassa ambaye alisema anasikia deko kutokana na wingi wa watu, alisema misamaha ya kodi kwa sasa ni Sh1.6 trilioni na kwamba atahitaji Sh1.3 trilioni kati ya hizo kwa ajili ya elimu itakayolipiwa na serikali kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Alirejea kusema kuwa katika serikali yake hakutakuwa na michango ya elimu, maabara wala madawati.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema viongozi waliokuwa CCM akiwamo Lowassa, wamejiunga na chama chao kwa kuwa kina misingi imara.
Akizungumzia suala la upigaji kura, alisema siku sita zilizobaki ni muhimu kwa Watanzania kufanya uamuzi na kusisitiza kuwa kuna kila sababu ya kubakia kwenye vituo vya kura baada ya kupiga kura huku akidai kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haiko huru.

Sumaye
Akihutubia mkutano huo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alimtaka Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe kuwasomea wananchi wa Mbeya, ripoti ya Richmond kuona kama Lowassa anahusika.
“Lowassa hahusiki, alijiuzulu kwa ajili ya kuwakoa wao na wao wanaendelea kuilipa Richmond kwa mgongo wa Dowans wakati Lowassa hayupo,” alisema.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alisema tatizo kubwa kwa wakazi wa jimbo lake ni maji hasa katika vijiji vya Uyole na Mwakibete na kusema kuna kila sababu ya kuvuta maji kutoka Ziwa Nyasa hadi Mbeya ili kukabiliana na tatizo hilo. Alisema matatizo mengine ni hospitali na huduma za afya akitaka wapatiwe mashine za x-ray, CT Scan na umeme wa uhakika.

Ilivyokuwa mchakamchaka
Kabla ya mkutano huo, Jiji la Mbeya lilitawaliwa katika hekaheka za mapokezi ya Lowassa kuanzia asubuhi huku wakazi wakianza kufurika kwenye uwanja huo tangu saa mbili asubuhi.
Jiji lilitawaliwa na pilipika za bodaboda na bajaji zenye bendera za Chadema katika maeneo mengi hususan Barabara Kuu ya Mbeya- Zambia kuanzia Kabwe, Mwanjelwa, Mafiati, Soweto na Mama John ulikofanyikia mkutano huo.
Wafuasi wa mgombea huyo walionekana wakirandaranda maeneo mengi ya jiji hilo wakiwa wamevalia sare za Chadema huku wakipiga deki Barabara Kuu ya Mbeya - Zambia.
Muda mfupi kabla ya mkutano kuanza, wafanyabiashara walifunga maduka kwenda kusikiliza sera.
Wachuuzi wa vyakula na vinywaji walihamishia biashara zao kwenye mkutano huo tangu usiku wa kuamkia jana na wengi walionekana kufurahia uamuzi wao kutokana na biashara waliyofanya.
Mmoja wa wauza chipsi, John Antony alisema: “Aisee si unajua tena kufaa kufaana, leo kuna neema kubwa kwetu ndiyo maana leo tumehamishia biashara yetu uwanjani.”
Mbarali
Katika mkutano wa Mbarali, wafuasi wa CUF na Chadema walizua tafrani wakati wakimsubiri Lowassa katika Uwanja wa Mpira, Rujewa.
Tafrani hiyo ilizuka baada ya mgombea wa CUF, Gamdust Haji kufika na gari lake kisha kushuka na wafuasi wanaomuunga mkono kwa kumbeba juujuu na kumpeleka jukwaa kuu, jambo ambalo liliwakera wafuasi wanaomuunga mkono mgombea wa Chadema, Liberatus Mwang’ombe na kutaka kumuondoa kwa nguvu.

Polisi wazima rabsha
Baadhi ya mashuhuda walisema kulikuwa na kundi la wafuasi wanaomuunga mkono mgombea wa CUF na kundi la mgombea wa Chadema ambao walikuwa wakilumbana huku kila upande ukitaka mgombea wao ndiye anadiwe na Lowassa kwa wananchi.
“Unajua hawa watu walishindwa kuafikiana nani agombee ubunge kupitia yale makubaliano yao Ukawa, kitu ambacho kila chama kilisimamisha mgombea wake,” alisema mmoja wa wakazi wa Rujewa mjini, Athumani Mwakitalima.
Akizungumzia suala hilo, Haji alisema: “Ni kweli nimefanyiwa vurugu, wamevunja vioo vya gari langu, wakitaka niondoke kwenye mkutano huo eti sina haki ya kushiriki na kumsikiliza mgombea wangu wa urais. Nimetoa taarifa polisi na kuna watu wamekamatwa.”
Aliwalaumu viongozi wa kitaifa walioambatana na Lowassa kwamba hawakutaka kuuliza sababu za yeye kutowapo mkutanoni hapo na badala yake kumnadi Mwang’ombe akisema hawakutenda haki.