Update:

JK: Miaka 10 inamtosha yeyote IkuluRais Jakaya Kikwete amesema kuwa miaka 10 inatosha kwa kiongozi kukaa Ikulu na kuwataka watumishi kumsaidia mrithi wake atakayechaguliwa katika Uchaguzi Mkuu Jumapili ijayo kwa ari zaidi ili kuchochea maendeleo ya taifa na kulifanya kuwa la kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania  
·         Asisitiza hahitaji muda wa ziada kuendelea kubaki Ikulu.
 

Rais alitoa wito huo Ijumaa iliyopita wakati wa hafla ya kuwaaga watumishi wa Ikulu, wakiwamo baadhi yao ambao wamedumu kwa kipindi chote cha miaka kumi ya uongozi wake. Aliwataka wafanyakazi hao kumpa ushirikiano rais huyo ajaye kuliko hata walivyofanya kwenye awamu yake ya uongozi na kumuunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yake ya ukuu wa nchi.

“Msaidieni rais ajaye kwa ari na nguvu zaidi kuliko hata mlivyonisaidia mimi katika uongozi wangu. Miaka 10 ya utawala inatosha kabisa kwa mkuu wa nchi kufanya mambo mengi na kumaliza ajenda zake. Sidhani kama mtu anahitaji zaidi ya muda kutekeleza yale ya msingi,” alisema Kikwete.
Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005 kuchukua nafasi iliyoachwa na mtangulizi wake, Rais Benjamin Mkapa ambaye naye alidumu kwa mihula miwili mfululizo.

Awali Rais Kikwete aliwashukuru watumishi hao na kusisitiza kuwa hahitaji muda wa ziada wa kuendelea kubaki Ikulu.
“Mzee Nyerere (Julius Kambarage, Rais wa kwanza na baba wa Taifa) alikaa miaka 23 na wala hakumaliza yote aliyoyakusudia. Wakati anaondoka, yaliyobaki alimwachia Mzee (Ali Hassan, rais wa awamu ya pili) Mwinyi ambaye naye alimwachia yaliyobakia Mzee Mkapa. Naye alifanya mengi lakini hakumaliza yote na akaniachia mimi. Na mimi nitamwachia rais ajaye,” alisema.
Kikwete amewaaga watumishi hao zikiwa zimesalia siku nne kufanyika Uchaguzi Mkuu huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekwishaeleza kwamba, ili kuondoa wasiwasi miongoni mwa wananchi, itatangaza mshindi wa urais kati ya siku tatu mpaka nne ingawa sheria inataka yatangazwe ndani ya siku saba.
Tofauti na chaguzi zilizopita, mwaka huu watu wengi zaidi wanatarajiwa kupiga kura baada ya kuonyesha nia tangu mchakato huo ulipoanza ikiwa ni pamoja na uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ambao ulifanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90 ya matarajio ya NEC.
Msisimko wa uchaguzi huo unaongezeka zaidi kutokana na ndoto ya kukua kwa uchumi kama ambavyo Rais Kikwete amewahi kunukuliwa akisema atakuwa rais wa mwisho kuitawala Tanzania maskini sambamba na kuibuka kwa uvumbuzi wa mafuta na gesi katika maeneo kadhaa nchini.
Rasilimali hizi zinategemewa kutimiza lengo la serikali kujiondoa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.