Update:

Busungu awanyooshea Mwantika, MaoMSHAMBULIAJI wa Yanga, Malimi Busungu, amesema beki wa Azam FC, David Mwantika na kiungo Himid Mao, wangemtoa roho kutokana na kumchezea rafu nyingi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa kila timu kushinda ili kujidhatiti kwenye kilele cha Ligi Kuu Tanzania Bara, ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Akizungumza na BINGWA juzi, Busungu alisema wawili hao walidhohofisha harakati zake za kuzifumania nyavu zao kutokana na kuchezewa rafu mara kwa mara.
Busungu alisema kama asingekuwa nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumtuliza hasira angeweza kuchukua uamuzi mbaya wa kushindwa kumvulia kile anachokuwa akifanyiwa na Mwantika.
Alisema kama michezo yote ingekuwa ikicheza hivyo, basi wachezaji wangelazimika kuingia uwanjani na silaha kwa lengo la kujihami.
Busungu alisema angeweza kupata kilema kutokana na rafu ambazo alikuwa akichezewa na wachezaji hao wa Azam.
“Kiukweli nilijikuta nikijiuliza maswali mengi juu ya Himid na Mwantika, hivi walitumwa kuja kunionyesha jinsi wanavyoweza kucheza rafu ili nipate kilema cha maisha?” alihoji.
Alisema aliomba mchezo umalizike haraka ili atoke, lakini alifurahi pale alipompisha Simon Msuva, kwani alishaona dalili zote za kuvunjika mguu.
Straika huyo amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wachezaji wote wakorofi na wanaocheza rafu mbaya uwanjani kwa sababu aina hiyo ya soka inaweza kuhatarisha maisha ya soka ya wachezaji wengi