Update:

Vyama vya siasa sasa vivunje majeshi yao
 Kuna habari kuwa Polisi imeonya vyama vya siasa vyenye majeshi. Onyo hilo lilitolewa juzi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu majukumu ya jeshi hilo kwa mujibu wa sheria na majukumu yake ya utendaji kazi.

Onyo hilo lilisisitizwa tena jana na Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Wote wawili, Paulo na Kova, walisema Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa vyama vyote vilivyo na vikundi vya ulinzi vyenye mwelekeo wa kijeshi, kuvunja vikundi hivyo mara moja, kwa vile vimekuwa vikiingilia majukumu ya jeshi hilo.
Walisisitiza kuwa jambo hilo ni kinyume cha sheria na Katiba ya nchi, inayolipa Jeshi la Polisi mamlaka ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Walitaja vikundi hivyo vyenye mwelekeo wa kijeshi, vinavyokwenda kinyume cha sheria kuwa ni Green Guard, Red Briged na Blue Guard.
Tunaunga mkono kauli hiyo ya makamanda hao wa Polisi, kwa sababu kuendelea kumiliki vikundi hivyo, kwa kisingizio chochote kile, ni uvunjifu wa Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa . Tunahimiza Jeshi la Polisi kutovumilia suala hilo liendelee.
Tuna imani Jeshi la Polisi nchini, litachukua hatua kali za kisheria kwa chama chochote, kitakachoendelea kukaidi amri hiyo. Kova alifafanua kuwa vikundi vya ulinzi vya vyama hivyo, vilipigwa marufuku na Jeshi la Polisi kwa sababu vinakwenda kinyume na Katiba ya nchi, inayolipa Jeshi la Polisi mamlaka ya ulinzi wa usalama wa raia na mali zao.
Lakini, pia alisema vikundi hivyo vinaweza kuwa na madhara baadaye. Tunakumbusha vyama vyote vya siasa nchini, vipatavyo 20, kuwa havina budi kutambua kuwa nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria na kwamba jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, ni la Jeshi la Polisi, siyo vyama vya siasa.
Vyama vya siasa nchini vikumbuke pia kuwa kuendelea kumiliki vikundi hivyo ni kwenda kinyume na agizo la Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) la kupiga marufuku vyama vya siasa kumiliki vikundi vya kijeshi.
Hata Msajili wa Vyama vya Siasa alishakataza vyama vya siasa kuwa na vikundi vyenye mwelekeo na kijeshi katika barua yake kwa vyama vya siasa nchini ya Machi 2 mwaka huu. Hatua za haraka hazina budi zichukuliwe kwa ajili ya kunusuru kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge, wawakilishi na madiwani zinazoendelea nchini kote, vinginevyo madhara yatakuwa makubwa hapo baadaye.
Chanzo: Habari leo newspaper