Update:

VYAKULA MUHIMU WAKATI WA UJAUZITOLishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana, kwani lishe hii hutumika kwa mama na mtoto anaendelea kukua tumboni. Kwa kawaida mahitaji ya chakula na virutubisho mwilini mwa mwanamke huongezeka wakati wa ujauzito na kadri ujauzito unavyoendelea kukua, virutubisho hivyo hutumika kujenga mwili wa mama na mtoto. Hivyo maamuzi ya lishe au lishe mama anayopata huathiri pia maendeleo ya mtoto anayekua mwilini mwake. Tutaona vyakula muhimu vya kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baadhi ya vitu vya kukwepa.

mjazito akipata mlo wenye mgoga za majani
Mlo kamili (balanced diet), ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazuri ya afya ya mjamzito na mtoto tumboni. Pamoja na mlo kamili mjamzito hupewa virutubisho ziada (supplements) kwa ajili ya kuongeza madini kama ya chuma na Foliki. Mlo kamili unajumuisha vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji kama inavyochambuliwa hapa chini;
Nafaka na Vyakula vya Wanga.
Vyakula hivi huupa mwili nguvu za kufanya kazi ikiwemo ukuaji wa mtoto tumboni. Vyanzo vya wanga ni kama nafaka mbalimbali(mahindi,mtama,ulezi n.k), viazi, ndizi, mihogo. Ni vizuri mjamzito awe anapata nafaka kamili(whole grains) kama mahindi, ngano na mchele usiokobolewa; cereals n.k. cereals
Nyama, Samaki na Vyakula vya Protini.
Hivi ni muhimu kwenye kuujenga mwili, hasa kipindi cha miwezi wa 4 mpaka wa 9 ambacho viungo mbalimbali vya mtoto vinajengwa. Ni muhimu mama apate vyakula vya protini vya kutosha ili kuhakikisha ukuaji wa mtoto unaenda vizuri. Nyama za kuku, ng’ombe, mbuzi, senene, panzi na wanyama wengine ; vyanzo vya protini za mimea kama maharage, soya, njugu, njegere, karanga,korosho n.k . Samaki, maziwa, mayai ni vyanzo vingine vya protini muhimu. vaykula vya protini
Vyakula vya Mafuta.
Hutumika kwenye kuupatia mwili nguvu pamoja na ujengaji wa seli za mwili. Mara nyingi vyakula kama nyama, karanga, ufuta, alizeti,senene, panzi, samaki na matunnda kama maparachichi huwa na mafuta. Ni vizuri kutumia mafuta yatokanayo na mimea ili kupunguza mafuta yenye lehemu(cholesterol) nyingi.
Mboga za Majani na Matunda.
Matunda na mboga za majani ni sehemu muhimu sana ya mlo wakati wa ujauzito, kwani huupatia mwili vitamini, madini na kambakamba kwa ajili ya kulainisha chakula. Vitamini husaidia kuimarisha kinga ya mwili sambamba na ufanyaji kazi wa mwili. Madini kama ya chuma, kalsiamu, zinki, madini joto(Iodine) na magneziamu ni muhimu kwa ukuaji salama wa mtoto tumboni mwa mama. mboga za majani
Vitamini B9 (Foliki asidi) na madini ya chuma hutolewa kama virutubisho ziada kliniki wakati wa ujauzito ili kutosheleza mahitaji ya mwili na kuzuia hatari ya upungufu wa damu kutokea.
Maji
Maji ni muhimu kwenye mmenyenyo na unyonywaji wa chakula, pia husaidia kuzuia choo kigumu, mwili kuvimba na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI). Inashauriwa mjamzito anywe maji si chini ya lita 2.3 kwa siku, yanaweza kuwa katika chai, juisi, soda, au maji yenyewe. Ni vema zaidi kama akinywa maji kama maji zaidi na kupunguza vinywaji kama soda.
Mfano wa Mpangilio wa Mlo.
Ili kuhakikisha mlo kamili mjamzito anaweza kufuata mfano wa mpangilio wa mlo ufuatao;
Mlo wa Asubuhi: A - Chungwa/ Embe/ Ndizi mbivu/ Parachichi, B - Mkate/ Maandazi/ Chapati/ Vitumbua,Uji C - Karoti D - Mayai, E - Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya
Mlo wa Mchana: A - Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na chungwa, B - Ugali/ Wali/ Ndizi/ Makande/ Tambi C - Mchicha/ matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji, D - Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa E - Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya Soya.
Mlo wa Usiku: A - Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na Chungwa, B - Wali/ Ndizi/ Viazi/ Tambi/ Chapati C - Mchicha/ Matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji, D - Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa E - Maziwa/Mtindi/Siagi/Maziwa ya Soya.
Vitu na Vyakula vya kuepuka/kupunguza ingawa hata jana tulivigusia pia
Matumizi ya Pombe wakati wa ujauzito huathiri mtoto. Haishauriwi kutumia pombe kabisa!
Uvutaji Sigara
Kupunguza unywaji wa kahawa au vinywaji vyenye caffeine nyingi.
Samaki aina ya papa, swordfish, tilefish na king mackerel kwani wana mekuryi kwa wingi amabayo ni mbaya kwa afya.