Update:

TAMBUA UGONJWA WA KIDOLE TUMBO(APPENDICITIS) NA TIBA YAKE


Kidole tumbo au Apendeksi hupatikana katika utumbo mkubwa, urefu wake ni kama kidole cha mwisho cha mkono, huwa hakina kazi yoyote mwilini. Sehemu hii hupitisha myeyuko wa chakula na endapo katika chakula hicho kuna michanga au vitu vidogovidogo vigumu, hujikita humo na kushindwa kutoka.

Kidole tumbo pia kinapatikana upande wa kulia wa tumbo kutoka usawa wa kitovu na nyonga ya kulia.

Taka ngumu hizo zikishajikita kwenye kidole tumbo na kushindwa kutoka ndipo kinapoanza kuvimba, hali hii kitaalam huitwa ‘Inflammation’. Hapa kidole tumbo kinavimba na kuwa na maumivu na pia hupata maambukizi ya bakteria.

Dalili za ugonjwa

Mgonjwa huanza kuhisi maumivu ya tumbo kuanzia usawa wa kitovu ambayo huwa makali na kuacha kisha kusambaa taratibu kuelekea upande wa kulia.

Baada ya muda mgonjwa huanza kutapika kisha kupata homa. Dalili hizi huwa haziji pamoja, huanza moja na kufuata nyingine lakini mgonjwa akiwahi kupata tiba dalili nyingine haziendelei. Baada ya hapo mgonjwa hupata homa.

Dalili za ugonjwa zinatofautiana kufuatana na aina ya ugonjwa huu ambapo kawaida umegawanyika katika hali ya ukali ‘Acute’ na hali ya usugu ‘chronic’. Maumivu makali yanayoambatana na homa na kutapika tunaita ni ‘Acute’

Maumivu ya ugonjwa huu ukifikia hatua mbaya husambaa hadi katika uti wa mgongo usawa wa kitovu au ‘Belly button’.

Pamoja na kwamba maumivu huanzia usawa wa kitovu, lakini dalili za awali kabisa huanzia juu ya kitovu ambayo huja na kupotea na mgonjwa anaweza kujihisi ana ugonjwa wa vidonda vya tumbo, baadaye ndipo hushuka chini taratibu na kusambaa.

Dalili hizi ni tofauti na watoto ambao hulalamika tumbo linauma sehemu zote kukiwa hakuna eneo maalam na baadaye maumivu huwa makali sana kwa tumbo lote hata akiguswa linauma sana.

Hali ya tumbo kuuma huambatana na kujaa gesi kwa wote yaani wanaume, wanawake na watoto.

Chanzo cha tatizo

Kama tulivyoona hapo awali chanzo cha tatizo, maumivu makali ‘Acute’ hapa hutokana na vile vitu vigumu vilivyoingia katika kidole tumbo kushindwa kutoka hivyo huziba kwa juu na zile taka ngumu huganda humo na kidole tumbo kuzidi kuvimba.

Hali ya usugu wa maumivu hutokana na taka ngumu hizo kukaa humo kwa muda fulani na baadaye hutoka huku ukiacha hali ya kidole tumbo kuwa na uvimbe.

Hali ya uvimbe ikikaa muda mrefu husababisha mzunguko wa damu kuzuiliwa sehemu hiyo hivyo kidole tumbo huvimba zaidi na husababisha kuta za Apendeksi kuharibika ‘Necrtotic’ na kukusanya majimaji kama usaha.

Hali hii husababisha tatizo liitwalo ‘Peritonitis’ yaani tumbo lote huathirika na kuuma. Mgonjwa akichelewa kupata tiba, usaha huu husambaa katika mfumo wa damu na kusababisha kifo.

Uchunguzi

Huzingatia historia ya mgonjwa, dalili na ishara zitajitokeza, vipimo vya damu vitafanyika, vipimo vingine ni vya Ultrasound na CT Scan ya tumbo vitasaidia kujua tatizo kwa undani zaidi.

Zipo pia njia mbalimbali za uchunguzi ambazo daktari anaweza kuzitumia mfano ‘Rovsing’s sign’ na sitokovkty’s sign na nyinginezo.

Matibabu
Tatizo hili katika hatua za awali mgonjwa anaweza kutibiwa kwa dawa lakini tatizo linapoendelea inabidi afanyiwe upasuaji kuondoa Apendeksi.

Tatizo likiwa kubwa, upasuaji wa dharura hufanyika. Ni vema uwahi hospitali kwa uchunguzi  tiba na dawa.
MKOMBOZI SANITARIUM CLINIC
0654361333